Mbunge wa Rombo, Joseph Selasini amewajia juu Mkuu wa
Wilaya ya Rombo, Lemrise Kipuyo na Mwenyekiti wa Halmashauri ya wilaya ya hiyo,
Anthony Tesha akiwataka wajiuzulu nyadhifa zao kwa kushindwa kusimamia sheria
wilayani humo.
Selasini alitoa kauli hiyo
jana alipokuwa akizungumzia
taarifa ya wanawake wa Rombo inayodai kwamba wanakodi wanaume kutoka Kenya ili
wafanye nao tendo la ndoa.
Juzi, gazeti hili liliripoti habari iliyomkariri Mkuu wa
Wilaya kuwa baadhi ya wanawake wilayani humo, hukodi wanaume kutoka Kenya kwa
ajili ya kufanya nao tendo la ndoa baada ya waume zao kupoteza nguvu kutokana
na ulevi.
Eneo ambalo limeathirika zaidi na unywaji wa pombe haramu
na zinazotengenezwa kiholela bila viwango ni la Kikelelwa lililopo mpakani mwa
Kenya na Tanzania.
Taarifa hiyo ilimnukuu Kipuyo wakati wa ufunguzi wa kikao
cha Baraza la Madiwani la Halmashauri hiyo na kuitaja Kikelelwa kama eneo
linalohitaji kutazamwa kwa jicho la pekee.
“Imefikia mahali wanaume wengi wanashindwa kumudu kufanya
tendo la ndoa na kuwalazimu wanawake wao kukodi wanaume kutoka nchi jirani ya
Kenya kwa ajili ya tendo hilo,” alisema Kipuyo.
Kauli hiyo iliungwa mkono na baadhi ya wanawake
waliozungumza mbele ya mkuu huyo wa wilaya katika operesheni ya kukamata pombe
haramu ya gongo kijijini hapo iliyofanyika wiki mbili zilizopita.
Jana, Selasini alikanusha vikali taarifa hizo akidai kuwa
siyo sahihi kuwajumuisha wanaume wote wa jimbo lake na ulevi huo au wanawake
wote.
“Hiyo kauli haina utafiti wala haijaonyesha ni wanaume
wangapi Rombo wana tatizo hilo au ni wanawake wangapi waume zao wana shida
hiyo. Siyo sahihi kutoa kauli ya jumla,” alisema.
Alisema, “Haiwezekani mtu mmoja aliyehojiwa akawakilisha
wanaume au wanawake wenye matatizo hayo. Kauli hiyo imewadhalilisha wanaume na
wanawake ambao hawahusiki na tatizo hilo.”
“DC ndiye mwenyekiti wa kamati ya ulinzi na usalama
aliyepaswa kusimamia sheria. Mwenyekiti wa halmashauri, naye anawajibika. Kama
wameshindwa kazi waachie ngazi.
“Siungi mkono unywaji holela wa pombe ambazo hazina
viwango vya TBS. Kama kuna mtu ana tatizo la tendo la ndoa ajitokeza tumjue.
Hili jambo limenifanya nipokea simu nyingi sana,” alilalamika Selasini.
Selasini alisema inawezekana hakuna mwananchi wake mwenye
tatizo hilo kwa vile hakuna utafiti wala majina ya waathirika na alimtaka
Kipuyo kuomba radhi kwa kauli yake hiyo.
Hata hivyo, Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro, Leonidas Gama
naye aliwahi kutoa kauli inayofanana na ya Kipuyo aliposema wapo baadhi ya
wanandoa wilayani humo wanalala “mzungu wa nne”.
MWANANCHI
No comments:
Post a Comment