Unadhani huyo mama katumia busara kumuuza mtoto kuliko kumtupa ama?
Mkazi mmoja wa Kijiji cha Nanja, Kata ya Lepruko,
wilayani Monduli, anadaiwa kumuuza mtoto wake wa kumzaa kwa mtu mwingine kwa
Sh70,000 kwa madai kuwa ana maisha magumu.
Katika tukio hilo la kushangaza, inadaiwa mwanamke huyo
(jina linahifadhiwa) aliamua kumuuza mtoto huyo wa kiume mwenye umri wa miezi
minane katikati ya Mei, mwaka huu akiwa ametoka naye mkoani Singida.
Mwenyekiti wa Kitongoji cha Nanja, Time Samsoni
akizungumza juzi mbele ya Mratibu wa Chama cha Wanawake Wanasheria Tanzania
(Tawla) Tawi la Arusha, Francisca Gaspar alisema walijaribu kumshawishi
akamchukue mtoto wake, lakini aligoma.
Mwenyekiti Samsoni alidai kuwa mtu aliyemnunua mtoto huyo
anaishi katika Kijiji cha Longonito na ana wadhifa mkubwa kijijini hapo.
“Kwa kweli tulisikitishwa na kitendo hicho cha huyo
mwanamke kumuuza mtoto wake kwa Sh 70,000 akisingizia maisha magumu na
ameshindwa kumlea,” alisema Samsoni.
Alisema walimwita mwanamke huyo kwenye ofisi ya kitongoji
na kumhoji sababu zilizomfanya amuuze mwanaye, lakini aliwaaambia kuwa hana
uwezo wa kumhudumia.
Mratibu wa Tawla, Gaspar alisema watahakikisha
wanafuatilia suala hilo ili lipatiwe mwafaka. “Lakini tumeambiwa kuwa mama huyo
ametoroka baada ya kuhojiwa na viongozi wa hapa kijijini na hajulikani aliko
mpaka sasa.”
Alisema katika kipindi hiki ambacho Tawla inaadhimisha
miaka 25 tangu ianzishwe, wanatoa elimu ya sheria kwa wanawake wa eneo la Nanja
na Meserani, hivyo jamii iwe inatoa taarifa kwao wanapoona matukio kama hayo.
Nina uhakika kuna matukio mengi yanatokea huku vijijini
ila taarifa zinashindwa kufikishwa na endapo mngetuarifu mapema,
tungeshirikiana na polisi huyo mama aliyemuuza mtoto wake angekamatwa kabla ya
kutoroka,” alisema Gaspar.
Mkazi mmoja wa eneo hilo, James Lengitambi alipongeza
hatua ya mwanamke huyo kumuuza mtoto wake kuliko angemtupa chooni au kwenye
mfuko wa Rambo kama wanavyofanya wanawake wengine.
“Tumezoea kusikia kwenye vyombo vya habari kuwa baadhi ya
wanawake wanawatupa chooni watoto wao au kuwatelekeza kwenye mifuko ya
plastiki, ila huyu amemuuza hajamuua,” alisema Lengitambi.
MWANANCHI
No comments:
Post a Comment