WAZIRI wa zamani wa Wizara ya Fedha, Basil Mramba, Waziri
wa Nishati na Madini, Daniel Yona na aliyekuwa Katibu Mkuu Wizara ya Fedha,
Gray Mgonja wamefunga utetezi na sasa wanasubiri hukumu ya mahakama.
Washtakiwa hao kupitia mawakili wao, Elisa Msuya na
Beatus Malimi waliiarifu mahakama hiyo jana mbele ya Jopo la mahakimu watatu
linaloongozwa na Jaji John Utamwa, kwamba kwa ushahidi uliotolewa hawaoni haja
ya kuita shahidi mwingine.
Jopo hilo ni Majaji John Utamwa, Sam Rumanyika na Saul
Kinemela.
“Tulitegemea kupata shahidi wa pili kwa ajili ya washtakiwa
lakini baada ya kuangalia ushahidi uliotolewa tumeona hatuhitaji shahidi
mwingine,”alidai.
Washtakiwa wote wanakabiliwa na kesi ya kutumia madaraka
vibaya na kuisababishia Serikali hasara ya Sh bilioni 11.7.
Wakili Msuya baada ya kufunga ushahidi huo kwa wateja
wake mshtakiwa wa kwanza na wa pili, aliomba kuwasilisha hoja za mwisho kabla
ya kutolewa hukumu.
Wakili Malimi alidai kwa upande wa mshtakiwa wa tatu
(Mgonja), pia wanaomba kufunga kesi yao. Baada ya kuomba kufanya hivyo, Jaji
Utamwa alisema kesi ya upande wa utetezi imefungwa.
Upande wa utetezi uliomba kuwasilisha majumuisho yao ya
mwisho, ambao walitakiwa kuwasilisha kwa pamoja kwa washtakiwa wote.
Wakili Msuya aliomba mahakama iwapatie mwenendo wa kesi
kwa upande wa utetezi na Wakili wa Serikali Mwandamizi, Shadrack Kimaro pia
aliomba kupatiwa mwenendo huo kwa ajili ya kuandaa majibu ya majumuisho ya
mwisho.
MTANZANIA
No comments:
Post a Comment