Raisi wa Zanzibar, Dr. Ali Mohammed Shein |
Polisi Zanzibar inawashikilia watu wawili kwa tuhuma za
kuwatukana na kuwakashifu viongozi wakuu wa serikali, akiwamo Rais wa Zanzibar,
Dk. Ali Mohammed Shein na Makamu wa Pili wa Rais, Balozi Seif Ali Iddi.
Akizungumza
na waandishi wa habari, Makao makuu ya Jeshi
la Polisi visiwani hapa, Naibu Mkurugenzi wa makosa ya jinai (DCI), Salum
Msangi, alisema watu hao wapo chini ya ulinzi
mpaka hapo upelelezi
utakapokamilika ili wafikishwe mahakamani. Aliwataja watu hao ambao ni wafuasi
wa Chama cha Wananchi (CUF) kuwa ni Said Ali Abdallah (26), aliyetoa maneno ya
uchochezi dhidi ya Rais wa Zanzibar na Makamu wa Pili wa Rais na watendaji wa
jeshi la polisi.
Alisema mtuhumiwa huyo alitoa maneno hayo na kusambaza
vitisho katika mitandao ya kijamii akisema endapo mwaka huu katika uchaguzi
mkuu CUF haitashinda, watachoma kambi na nyumba za jeshi hilo kisiwani Pemba.
Alimtaja mtuhumiwa mwingine kuwa ni Hussein Mageni
Hussein, maarufu Beko (27), ambaye
alimpigia simu Balozi Iddi na kumtukana na kumtumia ujumbe wa simu wenye
maneneo ya kashfa.
“Katika ujumbe wa sauti uliokuwa ukisambazwa na mtuhumiwa
Said Ali Abdallah alitoa onyo kwa viongozi wakuu akimtaka rais wa Zanzibar na
makamo wa pili wa rais wasiende Pemba kwani hakuna wafuasi wa chama chao na
kudai kuwa chama anachokishabikia ambacho ni CUF kisiposhinda kwenye uchaguzi
mkuu ujao atahamasisha wafuasi wezake wazitambue nyumba za askari polisi na
waziteketeze familia za askari hao,” alisema.
Alisema mtuhumiwa huyo alikamatwa kisiwani Pemba Mei 20,
na kuonekana kuwa watuhumiwa hao ni wahalifu wa kawaida wasio na msukumo wa
viongozi wa vyama vya siasa katika ushabiki wao.
Alisema baada ya kuwakamata watuhumiwa hao jambo
lililowashangaza, baadhi ya viongozi wa CUF na wanasheria wamekuwa mstari wa
mbele kuwashambilia wahalifu hao.
Alisema baada ya mtuhumiwa Said Ali kufikishwa makao
makuu ya polisi Zanzibar, Mwakilishi wa Jimbo la Kiwani, Hija Hassan Hija
(CUF), akiwa na mawakili watatu wa chama hicho walifika na kuanza kumtetea
mtuhumiwa huyo hata kabla hajaanza kuhojiwa.
Alisema hali hiyo inatoa picha kuwa watuhumiwa
wanashawishiwa na viongozi wa CUF
wakishirikiana na mawakili ili kuvuruga amani ya nchi. Alisema uchunguzi wa
awali, umebaini kuwa watuhumiwa wametenda makosa hayo kwani hata mawasiliano ya
simu waliyokuwa wakitumia yalichunguzwa na kujulikana ni wao na maeneo
wanayoishi.
“Simu walizokuwa wakitumia ni za mtandao wa Zantel na
tulifuatilia hadi katika kampuni ya mtandao huo na tukawabaini,” alisema.
NIPASHE
No comments:
Post a Comment