Waziri wa Ujenzi na Jeshi la Kujenga Taifa, Dk Hussein Mwinyi |
WAZIRI wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa, Dk Hussein
Mwinyi amesema vijana wote waliohitimu kidato cha sita mwaka 2013/14, 2014/15
na kutojiunga na mafunzo ya Jeshi la Kujenga Taifa (JKT) bila ridhaa ya jeshi
hilo, wanaendelea kusakwa na kuorodheshwa kwenye orodha ya watoro na upo
uwezekano wa wao kwenda mafunzo hayo mapema mwezi ujao.
Alisema kwa mwaka 2014/15 jumla ya vijana waliopata
mafunzo hayo kwa mujibu wa sheria ni 31,635 ambayo ni sawa na ongezeko la
vijana 15,632, ukilinganisha na vijana 16,003 waliohitimu mafunzo hayo mwaka
2013/14 .
“Hata hivyo idadi hiyo ni pungufu ikilinganishwa na idadi
ya vijana 41,000 waliohitimu kidato cha sita, waliostahili kujiunga na mafunzo
hayo, na sababu zilizofanya upungufu huo ni pamoja na kalenda ya awamu ya pili
ya mafunzo kugongana na kalenda ya kuanza mihula ya masomo ya elimu ya juu”,
alisema Dk Mwinyi.
Na kuongeza vijana waliopaswa kujiunga na mafunzo hayo
ila hawakujiunga bila ridhaa ya jeshi, wameingizwa kwenye orodha ya watoro wa
jeshi hilo na kwamba wizara inaangalia uwezekano wa kuiwezesha JKT, kuchukua
kundi hilo wakiwemo watoro, kuanza kwa mkupuo mmoja mafunzo hayo Juni hadi
Agosti mwaka huu.
“Tunatafuta uwezekano wa kuiwezesha JKT, kuwachukua
watoro wa mafunzo hayo na wale walioshindwa kujiunga kwa kugongana kwa mihula
ya masomo, kuingia mafunzoni kwa mkupuo mmoja kuanzia mwezi Juni hadi Agosti
mwaka huu, ili wawahi muhula wa masomo kwa elimu ya juu”, alisema Dk Mwinyi.
Hivyo aliwataka vijana wote waliohitimu kidato cha sita
na kupaswa kujiunga na JKT, na hawakufanya hivyo bila sababu wala kupata ridhaa
ya jeshi hilo wafahamu wako kwenye orodha ya watoro wa jeshi hilo na kwamba ni
lazima watapaswa kwenda mafunzoni.
HABARI LEO
No comments:
Post a Comment