Idadi ya watoto wanaozaliwa nchini Ujerumani imepungua
zaidi ya mataifa yote duniani.
Utafiti umeonesha kuwa idadi ya watoto wanaozaliwa nchini
Ujerumani ndiyo ya chini zaidi duniani na sasa kunahofu kuwa kupungua kwa uzazi
kutaathiri pakubwa uwezo wa vijana kuendeleza kasi ya ukuaji wa uchumi wa taifa
hilo tajiri zaidi barani Ulaya.
Watafiti wanaonya kuwa endapo jitihada mahsusi
hazitafanywa ilikuimarisha idadi ya watoto nchini humo basi uchumi wa taifa
hilo utaathirika vibaya.
Kulingana na utafiti huo,watoto 8.2 pekee walizaliwa
miongoni mwa watu wazima 1000.
Awali idadi ya chini zaidi ilikuwa ya Japan ambayo
huandikisha idadi ya watoto 8.4 wanaozaliwa miongoni mwa watu wazima 1000.
Kampuni ya uhasibu ya Ujerumani BDO ikishirikiana na chuo
cha utafiti wa kiuchumi cha Hamburg Institute of International Economics (HWWI)
ndiyo iliyoendesha utafiti huo kwa lengo la kutathmini uwezo wa uchumi wa taifa
hilo kujiendesha mbali na viwango vya uzazi vinavyoripotiwa nchini humo.
Barani Ulaya, Ureno na Italia ziliorodheshwa katika
nafasi ya tatu na nne zikiwa na jumla ya watoto 9.0 na 9.3 mtawalia.
Ufaransa na Uingereza zinasajili watoto 12.7 wanaozaliwa
miongoni mwa watu wazima 1000.
Niger iliyoko Afrika ndiyo inayoandikisha idadi kubwa
zaidi ya watoto wanaozaliwa duniani.
Nchini humo watoto 50 huzaliwa miongoni mwa watu wazima
1000.
Kulingana na utafiti huo wa BDO iwapo hali itaruhusiwa
kuendelea hivyo basi idadi ya watu wenye umri wa kati ya miaka 20 na 65 wenye
uwezo wa kufanya kazi na uwezo wa kuendesha uchumi wa taifa hilo itapungua kwa
asilimia 61% hadi 54% ifikapo mwaka wa 2030.
Aidha afisa wa BDO Arno Probst, aliwatahadharisha wajerumani
kuwa kiwango cha malipo na mishahara ya wafanyikazi kitaongezeka maradufu kadri
ya upungufu wa watu wenye uwezo wa kufanya kazi .
Probst alisema Ujerumani italazimika kuwaruhusu wahamiaji
kuingia nchini humo na kufanya kazi ilikuepuka kuzorota kwa uchumi wake.
BBC
No comments:
Post a Comment