ASKARI wa Jeshi la Kujenga Taifa (JKT), aliyefahamika kwa
jina la Ramadhani Hamisi (24), anadaiwa kumuua mkazi wa Mikanjuni, mkoani
Tanga, Salim Omary (21).
Tukio hilo linadaiwa kutokea Mei 17,
mwaka huu, wakati
marehemu na mtuhumiwa wakiwa kituo cha kujiandikisha kwa ajili ya kupatiwa
vitambulisho vya uraia ambavyo vinatolewa na Mamlaka ya Vitambulisho vya Taifa
(NIDA).
Mtuhumiwa Hamisi anadaiwa kumpiga ngumi Salim Omary
aliyekuwa akiamulia ugomvi uliotokea kati ya askari huyo na mama mmoja ambaye
jina lake halikufahamika.
Akithibitisha kutokea kwa tukio hilo, Kamanda wa Polisi
mkoani humo, Zubery Mwombeki, alisema lilitokea saa 9:30 alasiri katika Shule
ya Msingi Mikanjuni, Kata ya Mabawa, ambako kulikuwa na kituo hicho.
Alisema baada ya mama huyo kulalamika kuwa amekaa muda
mrefu kituoni hapo bila kupata huduma ndipo ukatokea mzozo kati yake na askari
huyo ambapo Salim iliingilia ili kuwaamua lakini akajikuta akipigwa ngumi ya
kichwani na mbavuni.
"Marehemu alikimbizwa katika Kituo cha Afya
Mikanjuni kwa ajili ya matibabu lakini jitihada za madaktari na wauguzi kuokoa
maisha yake zilishindikana ambapo maumivu makali aliyopata ndiyo
yaliyosababisha kifo chake," alisema.
Aliongeza kuwa, askari huyo anashikiliwa na jeshi hilo na
atafikishwa mahakamani muda wowote.
Kwa upande wake, Naibu Meya wa jiji hilo ambaye ni Diwani
wa kata hiyo, Mzamin Shemdoe, alidai kupata taarifa za tukio hilo baada ya
kupigiwa simu na wananchi wake.
"Nimepigiwa simu kuambiwa kuna askari wa JKT
amempiga raia ngumi ya mbavu na kichwa baada ya kutokea mgogoro, tukio hili
limenisikitisha sana," alisema.
MAJIRA
No comments:
Post a Comment