Askofu wa Kanisa la Ufufuo na Uzima, Josephat Gwajima,
jana aliibukia kwenye mkutano wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema),
Jimbo la Kawe, Dar es Salaam.
Mkutano huo ulikuwa wa uzinduzi
wa kitabu cha kazi
alizofanya Mbunge wa jimbo hilo na Mwenyekiti wa Baraza la Wanawake wa Chadema
(Bawacha), Halima Mdee.
Askofu Gwajima alionekana kwenye jukwaa kuu na viongozi
mbalimbali wa Chadema, akiwamo mwenyekiti wa chama hicho, Freeman Mbowe, katika
mkutano uliofanyika katika viwanja vya Tanganyika Packers, Kawe, jijini Dar es
Salaam.
Miongoni mwa watu wengine
maarufu waliokuwapo kwenye mkutano huo ni mwimbaji wa nyimbo za injili,
Flora Mbasha, ambaye aliimba wimbo maalum kwa ajili ya chama hicho na
ulizinduliwa jana.
Mkutano huo ulitanguliwa na maonyesho ya kikundi cha
ulinzi cha Chadema (Red Brigade) na
baadaye wimbo maalum wa amani na pongezi kwa chama hicho ulioimbwa na Mbasha na
kuamsha shamrashamra kwa watu waliohudhuria ikiwamo kupanda jukwaani kucheza.
HOTUBA YA MBOWE
Mwenyekiti wa Chadema Taifa, Mbowe, akihutubia mamia ya
wananchi wa jimbo hilo, alisema uchaguzi wa mwaka huu ndiyo matamanio ya baba
wa Taifa, Hayati Mwalimu Julius Nyerere, ambayo alikuwa nayo wakati wa siku za
mwisho za uhai wake.
“Mwalimu Nyerere alisema: “Watanzania wanataka
mabadiliko, wasipoyapata ndani ya CCM watayatafuta nje ya CCM,” sasa wakati wa
kuyatafuta nje ya CCM umefika na
Watanzania kwa kushirikiana na Ukawa na wananchi wasio na chama lakini wana
mapenzi mema na nchi wanaungana nasi.”
Mbowe alisema baada ya kutembea nchi nzima amegundua
Watanzania wanayataka mabadiliko, wana uwezo wa kuyaleta na wako tayari
kuyaleta, utayari ambao hauipi amani CCM na kudai ndiyo maana ina haribu mfumo
wa uandikishaji wapigakura katika Daftari la Kudumu la Wapiga Kura kwa mfumo wa
Biometric Voters Registration,” alisema.
AIPOPOA MAWE NEC
Alisema juzi alitembelea vituo vya uandikishaji mkoani
Mbeya katika wilaya ya Rugwe Tukuyu, Kyela na alibaini Watanzania wanalala
kwenye vituo vya kujiandikisha kwa sasabu vifaa havitoshi na imefanyika hivyo
makusudi ili Watanzania wengi wasiandikishwe.
“Naomba kupitia mkutano huu nimshauri Mwenyekiti wa Tume
ya Taifa ya Uchaguzi (Nec), Jaji Damian Lubuva, lawama utakayoipata kutokana na
BVR, CCM hawatakuwa na wewe, wanakutumia kwa sasa, kikiwaka utawekwa kando,”
alitahadharisha na kuongeza:
“Vifaa (BVR Kits) havitoshi, tunakuomba (Jaji Lubuva)
utangaze umeongeza siku za kujiandikisha na siyo siku saba ili wenye sifa
wajiandikishe.
“Nimeshuhudia kinamama wanalala vituoni kwa sababu
uandikishaji umekuwa adhabu kwao,” alidai.
Mwenyekiti huyo wa Chadema ambaye pia ni Mwenyekiti wa
Ukawa, alisema wapigakura wengi wanaunga mkono mabadiliko na wakijiandikisha
itakuwa ni kaburi kwa CCM na kuongeza:
“Jaji Lubuva
kaburi ulilobeba ni lako mwenyewe, tunakuomba uongeze siku za kuandikisha
wapiga kura.”
Mbowe alisema uchaguzi mkuu kikatiba unatakiwa kufanyika
Oktoba 25, mwaka huu na kwamba kwa sasa zimebaki siku 121 kufika siku hiyo na
Nec haijatangaza majimbo ya uchaguzi na uwakilishi pamoja na ratiba ya
uchaguzi.
“Wajiandae kisailokijia kuachia madaraka ya nchi,
mnachelewesha uandikishaji wa wapiga kura ili wengi wasijiandikishe zimebaki
siku chache utawala uliopo kwa sasa uondoke madarakani,” alisema Mbowe ambaye
hotuba yale ilikuwa inarushwa moja kwa moja na kituo cha ITV.
Kwa mujibu wa Mbowe, serikali itakayoundwa na Ukawa
itaongoza taifa katika misingi ya kurudisha utawala wa haki na sheria ili
kurudisha matumaini kwa wananchi wote.
Aidha, aliwataka watumishi wa umma kutokuwa na hofu kwani
Ukawa haingii kubadili au kufukuza mtu kazi, bali kufanya mabadiliko makubwa
kwa Watanzania na kwamba kitakachobadilika ni vyama vinavyoongoza nchi na siyo
mifumo ya utawala.
MISWADA YA HABARI
Mbowe ambaye pia ni Kiongozi wa Kambi Rasmi ya Upinzani
Bungeni, alisema Mswada ya Sheria ya Huduma za Vyombo vya Habari na Muswada wa
Sheria ya Haki ya Kupata Habari 2015, ikifikishwa bungeni mwaka huu, wabunge wa
Ukawa watasimamisha Bunge na hawatakubali kuipokea.
“Ndani ya Muswada wa Sheria ya Huduma za Vyombo vya
Habari uhuru wa kupata habari unataka ikifika saa mbili usiku, vyombo vyote vya
habari binafsi ni lazima vijiunge na TBC One kusikiliza na kutazama taarifa ya
habari, huu ni ukandamizaji na haikubaliki,” alisema huku akishangiliwa.
“Kupitia mkutano huu nawaambia siku serikali italeta
miswada hiyo, tutasimamisha Bunge halitaendelea kwa sababu huwezi kufanya
uporaji wa haki kwa kiasi hicho,” alisema.
Aidha, alisema Muswada wa Sheria ya Makosa ya Mtandaoni
2015, uliopitishwa katika Mkutano wa 19 wa Bunge una vifungu visivyofaa na kwamba
utawala utakaokuja hautaki sheria za kuminya uhuru wa watu na kwamba kama rais
amesaini zitabaki ‘kapuni’ iwapo Ukawa wataingia madarakani.
Mbowe aliwataka wakazi wa jiji la Dar es Salaam
kujiandikisha kwa wingi ili kufanya mabadiliko nchini kwa kuwa jiji hilo ndilo
lenye wapigakura wengi.
Alisema licha ya kasi kubwa ya maendeleo na ukuaji wa
jiji, lakini wananchi wanaishi maeneo ambayo hayajapimwa kwa kuwa marais watatu
waliopita akiwamo Rais Jakaya Kikwete hawajafanya mipango miji na kwamba Mwalimu
Nyerere alifanya ya kwanza wakati jiji likiwa na wakazi 275,000 na mara ya pili
likiwa na wakazi 750,00.
Mwenyekiti huyo alisema kwa kasi ya ukuaji wa jiji na
mpango wa ujenzi wa barabara za mabasi yaendayo kasi havilingani kabisa.
Kuhusu huduma ya majisafi na salama, alisema ni asilimia
nane ya wananchi ndiyo wanaopata maji safi na salama, asilimia 80 wanatumia
maji ya visima ikiwa ni miaka 51 ya Uhuru. Alisema jiji hilo ndiyo sehemu pekee
ambako mtu anaweza kukaa kwenye foleni kwa saa sita, jambo ambalo linaonyesha
utawala uliopo umeshindwa na nchi haiwezi kuendelea kwa kuwa na utawala wa aina
hiyo.
Mbowe alisema kuna dalili za wazi za serikali iliyopo
kuchoka kwa kuwa kwa sasa kuna migogoro mikubwa baina ya serikali na madereva,
watu wenye ulemavu, wanafunzi wa vyuo vikuu, wakulima na wafugaji.
ASKOFU GWAJIMA
Akizungumza na hadhara hiyo baada ya Mbowe kumaliza
kuhutubia, Askofu Gwajima alisema hotuba ya Mbowe ina ujumbe mzito na kwamba
ana amini aliyozungumza kaongozwa na Mwenyezi Mungu kuyazungumza kwa ajili ya
umma.
Alisema anatambua kuwa Chadema ina thamini mabadiliko na
kutoa baraka kwa chama hicho kuendelea na jitihada hizo kwa kuwa wakati wa
ukombozi umewadia.
MNYIKA: WANAWAKE JITOKEZENI KUGOMBEA
Awali, Naibu Katibu Mkuu wa Chadema Bara, John Mnyika,
aliwataka wanawake kujitokeza kugombea nafasi mbalimbali nchini katika uchaguzi
mkuu ili kuongoza mabadiliko nchini kama alivyofanya Mdee katika jimbo hilo.
Alisema kinamama wana majukumu mengi, wanahangaika na
shida katika huduma za afya, kuhudumia familia, kupata maji na mahitaji mengine
muhimu ya familia, lakini wapo ambao wamejitokeza kwenye nafasi mbalimbali za
uongozi na kufanya vizuri.
Mbunge Mdee akihutubia umati wa wananchi waliohudhuria,
alisema alimkaribisha Mbasha Chadema na kwamba ni nyumbani kwa kuwa aliumia
sana alipomkosa ndani ya chama hicho.
Aidha, aliwakaribisha wasanii wengine kujiunga na chama
hicho kwa kujitokeza hadharani kama alivyofanya Mbasha.
Mdee aliwashukuru wananchi wa Kawe kumuweka katika ramani
ya Tanzania na kwamba ni lazima kukiondoa Chama Cha Mapinduzi (CCM) madarakani
kwa kuwa kimeshindwa kutekeleza mahitaji ya Watanzania.
Aidha, alisema wanawake wa Tanzania wanateseka kwa kukosa
huduma muhimu za kijamii ufisadi umekithiri ndani ya serikali.
CHANZO: NIPASHE
No comments:
Post a Comment