BERNAD MEMBE, WARIZI WA MAMBO YA NJE NA USHIRIKIANO WA KIMATAIFA |
KATIKA hali isiyokuwa ya kawaida, mamia ya wanafunzi wa
Kitanzania wanaosoma katika shule za msingi nchini Kenya, wameripotiwa
kufukuzwa nchini humo.
Tayari 50 kati yao, wamerejeshwa
nchini huku wengine
kadhaa wakiwa bado wamekwama katika eneo la Narok Magharibi. Baadhi ya
walioathirika ni wale ambao wako katika hatua za mwisho za kuhitimisha elimu
yao ya msingi katika darasa la nane.
Mkuu wa Wilaya ya Ngorongoro, Hashim Mgandilwa alikiri
kuwepo na tatizo hilo na alilieleza gazeti hili jana kuwa: “Ni kweli wanafunzi
wetu waliokuwa wanasoma Kenya wamefukuzwa nchini humo na 44 kati yao
wamesharudi nchini, ila tuna wasiwasi kwamba mamia wengine watakuwa bado
wamekwama huko na tuko mbioni kuwafuatilia zaidi.”
Meneja wa Baraza la Wafugaji katika Tarafa ya Ngorongoro,
Peter Metele naye alikiri kuwepo kwa tatizo hilo na kuongeza kuwa yeye ndiye
anayefanya kazi ya kwenda kuwachukua wanafunzi waliotimuliwa Kenya.
Imeelezwa kuwa chanzo cha kutimuliwa kwa watoto hao ni
msuguano, ulioibuka baada ya kufanyika kwa operesheni maalumu ya kuwaondoa
wahamiaji haramu kutoka nchi jirani ya Kenya, wanaodaiwa kuvamia maeneo ya
Loliondo na Sale.
Hadi sasa watoto 27 wamehifadhiwa kwenye nyumba ya kulala
wageni ya Cobra katika eneo la Wasso, Loliondo. Wengine takribani 10 wamepelekwa
kwenye kata ya Arash na waliobakia wako majumbani mwao.
“Tumewahifadhi kwenye nyumba za kulala wageni kwa sababu
kuna wale wanaotoka vijiji vya mbali sana na tunataka tujitahidi kufanya
mazungumzo na viongozi wa upande wa Kenya ili waruhusiwe kurejea mashuleni,
iwapo tutafanikiwa basi iwe rahisi kuwarudisha Kenya,” alisema Mwenyekiti wa
Baraza la Wafugaji wa Ngorongoro, Metili.
Imedaiwa kuwa wanafunzi waliofanikiwa kurejeshwa ni wale
wanaodhaminiwa na Baraza la Wafugaji na wale waliopelekwa na taasisi mbalimbali,
ambao ilikuwa rahisi kutumiwa usafiri, ila kwa waliopelekwa na wazazi wao, bado
wamekwama Kenya.
“Tulishafanya mazungumzo ya awali na viongozi wa upande
wa Kenya siku ya tarehe 12 Mei mwaka huu, lakini ingawa tulikubaliana mengi,
ikiwemo wafanyabiashara wetu kuruhusiwa kupeleka bidhaa Kenya inaonekana kuwa
wananchi wa Narok wao wana maamuzi yao tofauti na serikali yao hivyo
wanasisitiza kuendeleza mzozo, na sasa wameamua kuongeza tatizo kwa kuwatimua
watoto,” alisema Mkuu huyo wa Wilaya.
Kwa upande wake, Katibu wa Baraza la Wafugaji,
Ngorongoro, James ole Moringe alisema baraza hilo pia linafanya jitihada za
kukutana na viongozi wa Narok na walimu wa huko ili kupata mwafaka wa suala
hilo.
Akisimulia, mmoja wa wanafunzi hao, Lilian Peter (14) anayesoma
darasa la Nane katika Shule ya Ilkerin-Loita, alisema Chifu wa eneo hilo
alifika shuleni kwao na kuwaita walimu ofisini, kisha baadaye Mwalimu Mkuu,
Abel Githinji alianza kuingia madarasani na kuwatoa wanafunzi wote wa
Kitanzania huku akiwaagiza wafungashe virago.
Wengi wa wanafunzi hao ni wale wanaotoka kwenye tarafa
mbalimbali za wilaya ya Ngorongoro, ambayo imepakana moja kwa moja na Kaunti au
Jimbo la Narok, Kenya.
Mwanafunzi mwingine, Naini Petey ambaye anasema wenzao
wanaosoma shule nyingine ya Naikara, pia walifukuzwa na wengi wao bado
wamekwama nchini Kenya, wakisubiri wazazi au wafadhili waende kuwachukua.
Juhudi za gazeti hili kuwapata mawaziri wenye dhamana ya
mahusiano ya kimataifa, Bernard Membe wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano
wa Kimataifa na Dk Harrison Mwakyembe wa Wizara ya Ushirikiano wa Afrika
Mashariki, hawakupatikana katika ofisi zao, kwa njia za simu na hata bungeni
Dodoma kuweza kuzungumzia suala hilo.
HABARI LEO
No comments:
Post a Comment