Saturday, May 23, 2015

Selasini ajipalia mkaa kuhusu wanawake Rombo na pia ombi la gongo ihalalishwe

Mbunge wa Rombo, Joseph Selasini
Mbunge wa Rombo, Joseph Selasini amejipalia makaa kwa kukanusha taarifa za wanaume wa jimbo hilo  kupoteza nguvu za kufanya tendo la ndoa kutokana na ulevi. Pia kauli ya kumtaka Waziri Mkuu, Mizengo Pinda atumie nafasi yake kuhalalisha biashara ya pombe haramu ya gongo kwa madai kuwa inawaingizia kipato watu wa hali ya chini imelaaniwa.

Mkuu wa Mkoa Kilimanjaro,
Leonidas Gama, baadhi ya wasomi na wananchi, wamesema Selasini hajui ukweli wa tatizo hilo bali amekurupuka kulikanusha wakati liko wazi.

Baadhi ya viongozi wa dini wa Kanisa Katoliki jimboni humo, wamekiri wanawake kutopatiwa haki yao ya msingi kwa muda mrefu, huku idadi ya watoto ikipungua.

Juzi, Gama alifanya ziara katika Kijiji cha Kikelelwa kilichoathiriwa zaidi na tatizo hilo.

Katika ziara hiyo, wakazi wa eneo hilo walimlaumu mbunge wao kwa kuingiza siasa katika janga linalotafuna maisha ya watu wake.

“Wananchi wanakubali pombe hizo zinaharibu nguvu za kiume na wanawake wamekiri kuwa wanakaa miezi tisa bila kupewa huduma ya ndoa halafu kiongozi anasimama anasema ni uongo,” alisema Gama na kuwataka wananchi kutompa kura kiongozi anayetaka gongo ihalalishwe wakati tayari imeleta madhara makubwa katika familia nyingi jimboni humo.

MWANANCHI

No comments:

Post a Comment