Wazri Mkuu Mizengo Pinda amewataka Watanzania wote
wajenge tabia ya kuandika wosia ili kuondoa matatizo ya mirathi pindi mwenza au
mme anapoaga dunia.
Alitoa wito huo jana wakati akizindua kampeni
ya kuandika wosia
kwenye maadhimisho ya miaka 25 ya Chama cha Wanasheria
Wanawake Tanzania (Tawla) yaliyofanyika, jijini Dar es Salaam.
Akizungumza mara baada ya kushuhudia uandishi wa wosia
mbele ya wakili, Waziri Mkuu alisema uandishi wa wosia ni suluhisho la migogoro
mingi inayosababishwa na wanandugu ambao wakati mwingine wala hawakushiriki
kuchuma mali wanayogombea.
“Kuandika wosia siyo uchuro kama ambavyo watu wengi
wanadhani… ninatoa kwa Watanzania kuandika wosia mapema kwani inasaidia kuondoa
matatizo ya mirathi baada ya mmoja wao kuondoka duniani,” alisema.
“Mtu anapaswa kutamka mali nilizonazo ni kadhaa na endapo
nitakufa mali hii apewe fulani, na hii fulani na nyingine fulani. Hati hii
inapaswa kutunzwa kwa mwanasheria, benki au kwa Kabidhi Wasii. Tusipolifanya
hili, matatizo yataendelea kuwakumba wajane na watoto walioachwa na marehemu,”
alisema. Aliipongeza Tawla kwa kuchukua jukumu la kuhamasisha umma kuhusu suala
la uandishi wa wosia lakini pia akawataka wanachama wake wajikite zaidi
kwenye kutetea haki za makundi maalum kama walemavu wa ngozi, vikongwe na watu
kutoka makabila madogodogo.
“Haya makundi yana shida zao ambazo hazifanani na
watu wengine. Nendeni vijijini, mkatoe elimu, jueni changamoto wanazokabiliana
nazo, wasikilizeni shida zao na muone ni njia gani mnaweza kuwasaidia,” alisema.
CHANZO: NIPASHE
No comments:
Post a Comment