Tuesday, May 26, 2015

INASIKITISHA SANA! Mtoto Alawitiwa na Kuuawa Kilimanjaro....Kisha Akakatwa Sehemu za Siri

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kilimanjaro, Fulgence Ngonyani
WATU watatu wamefariki dunia mkoani Kilimanjaro, katika matukio matatu tofauti, likiwemo la mtoto aliyetambulika kwa jina la Faterine Massawe (14) kulawitiwa na kuuawa kikatili, kisha kukatwa sehemu zake za siri na ulimi na watu wasiojulikana.

Wakizungumza na gazeti hili, baadhi ya wananchi walioshuhudia mwili wa marehemu ukiwa umetelekezwa katika shamba la watawa la Kanisa la Katoliki mjini Moshi, walidai mwili wa mtoto huyo ulikutwa ukiwa hauna nguo hata moja, huku sehemu yake ya siri ikionekana kuingiliwa kinyume na maumbile.

Mmoja wa wananchi hao, Alex Mushi alidai mwili wa marehemu unaonekana kuwa na majeraha makubwa, ikiwa ni pamoja na kwenye paji la uso, kuonesha alipigwa na kitu kizito ambacho kilisababisha kifo chake.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kilimanjaro, Fulgence Ngonyani, alithibitisha kuwapo kwa matukio hayo.

Alieleza kuwa tukio la kuuawa kwa mtoto huyo lilibainika baada ya maiti kuokotwa Mei 23 majira ya saa 1:00 asubuhi katika eneo la kata ya Karanga Manispaa ya Moshi.

Kamanda Ngonyani alisema mtoto huyo ametambulika kuwa ni mwanafunzi wa darasa la nne katika shule ya msingi Karanga mjini Moshi na kwamba maiti alipatikana baada ya kupotea nyumbani kwao tangu Mei 21 mwaka huu majira ya saa tisa alasiri, akiwa na mtu mmoja, Mark Ulomi (50) mkazi wa barabara ya Kibosho.

Alisema Jeshi la Polisi limefanikiwa kumkamata mtuhumiwa aliyedaiwa kuonekana naye na linaendelea na upelelezi kubaini chanzo cha mauaji hayo. Mwili wa marehemu umehifadhiwa Hospitali ya Mkoa ya Mawenzi kwa uchunguzi zaidi.

HABARI LEO

No comments:

Post a Comment