MTOTO wa kike mwenye umri wa miaka tisa ameonesha ujasiri
wa kipekee kwa kumwokoa mama yake mzazi, Magreth Ibrahim (50) kuuawa na mamba
baada ya kupambana na mnyama huyo kwa zaidi ya nusu saa.
Mama huyo mkazi wa kijiji cha Karema,
mwambao mwa Ziwa
Tanganyika wilayani Mpanda, kwa sasa amelazwa katika Hospitali ya wilaya ya
Mpanda mjini Mpanda kwa matibabu baada ya mkono wake kunyofolewa na mamba
aliyemshambulia wakati akifua kando ya Mto Ikola.
Akimweleza Mkuu wa Wilaya ya Mpanda, Paza Mwamlima aliyemtembelea
hospitalini hapo masaibu yaliyomsibu, alisema anamshukuru sana binti yake
mwenye umri wa miaka tisa aliyeweza kuokoa maisha yake licha ya kuwa
amenyofolewa mkono na mamba huyo.
Akisimulia mkasa huo, Magreth alieleza kuwa juzi akiwa
anafua kando ya mto Ikola ghafla mnyama huyo aliibuka majini na kumpiga usoni
na mkia wake.
“Mamba huyo aliibuka ghafla mtoni na kunichapa usoni na
mkia wake nami nikaangukia majini ndipo aliponidaka mkono wangu na kunivutia
mtoni ….binti yangu aliyekuwa jirani yangu alipoona niko karibu kuliwa na mamba
kwa ujasiri aliweza kukabiliana naye … Alinishika mkono mwingine na kunivutia
nje huku akipiga kelele kumtisha mnyama huyo ili aniachie hatimaye akaunyofoa
mkono wangu na kutokomea nao mtoni ….” alieleza.
Aliongeza kuwa watu waliokuwa wakifua mtoni hapo wengi
wao wakiwa wanawake walifika eneo la tukio ambapo wakiwa na binti yangu
walimvuta na kumtoa nje na baadae wakamkimbiza hospitalini mjini Mpanda kwa
matibabu.
Naye Kaimu Mganga Mkuu wa Wilaya ya Mpanda, Dk Joseph
Mkemwa amethibitisha kuwa hali ya mama huyo inaendelea kuimarika baada ya
kupatiwa matibabu.
HABARI LEO
No comments:
Post a Comment