MFANYABIASHARA maarufu wa madini ya Tanzanite, mkazi wa
Arusha, Eliakimu Daud Molle (45), amepandishwa kizimbani katika Mahakama ya
Hakimu Mkazi Arusha akikabiliwa na shtaka la kutapeli na kujipatia madini yenye
thamani ya sh. milioni 15 kwa njia ya udanganyifu.
Mshtakiwa alifikishwa mahakamani
hapo mwishoni mwa wiki
iliyopita mbele ya hakimu, Nestory Baro ambapo Mwendesha Mashtaka wa Serikali,
Gaudencia Lyimo, aliieleza mahakama hiyo kuwa mshtakiwa alitenda kosa hilo
Januari 4, mwaka huu, katika Jengo la Ottu.
Alisema mshtakiwa alijipatia madini ya Tanzanite kutoka
kwa mlalamikaji, Banai Shininu yenye thamani kiasi hicho baada ya
kumrubuni kuwa ampatie ili akayauze kwa sh. milioni 15
lakini hakufanya hivyo badala yake alitoweka kusikojulikana.
Aliongeza kuwa, mshtakiwa alikuwa akitafutwa muda mrefu
na mlalamikaji ambapo anapopatikana, hutoa ahadi za uongo kuwa angelipa fedha
hizo lakini hakufanya hivyo hadi alipokamatwa na kufikishwa mahakamani.
Baada ya kusomewa shtaka hilo, mshtakiwa alikana ambapo
Baro alisema dhamana ipo wazi kwa masharti ya kuwa na fedha taslimu sh. milioni
7.5 na wadhamini wawili lakini mshtakiwa alishindwa kuyatimiza na kupelekwa
gerezani.
Kesi hiyo namba 88 ya mwaka huu, imepangwa kutajwa tena
mahakamani hapo Mei 26, mwaka huu.
MAJIRA
PICHA: MITANDAONI
No comments:
Post a Comment