IDADI ya wagonjwa ambao wameugua ugonjwa wa ajabu katika
kata 6 za wilaya ya Meatu mkoani Simiyu imezidi kuongezeka hadi kufikia 1,048.
Mganga Mkuu wa wilaya ya Meatu,
Dkt. Adamu Jimisha,
alisema kwamba awali wagonjwa waliokuwepo ni 80
lakini idadi imeongezeka hadi kufikia 1,048 ambao walifikishwa kituo cha afya
Mwandoya.
Dkt. Jimishi alitoa taarifa hiyo jana mbele ya kamati ya
ulinzi na usalama ya Mkoa, iliyoongozwa na Mkuu wa Mkoa, Elaston Mbwilo, wakati
ilipowatembelea baadhi ya wagonjwa waliolazwa katika kituo hicho cha afya
pamoja na kata za Mwabusalu, Lingeka, Mwakisandu, Tindabuligi na Lubiga ambazo
zimekumbwa na ugonjwa huo.
Alisema bado hali za baadhi ya wagonjwa zimeendelea
kubaki zile zile, ambazo ni kuumwa kichwa, kikohozi kikavu, mwili kulegea,
kuchanganyikiwa akili pamoja na kupoteza fahamu.
Aliongeza kuwa wagonjwa hao wanatibiwa na kuruhusiwa
kwenda nyumbani pindi wanapopata nafuu au kupona kabisa. Alisema baadhi yao
walikutwa na magonjwa mbalimbali kama malaria na minyoo.
Alisema wataalam wa Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii
wakiambatana na timu ya Mkoa akiwemo Mganga Mkuu wa Mkoa, Mtaalam wa Maabara na
Daktari mmoja walichukua sampuli kwa ajili ya kupelekwa Nairobi kwa uchunguzi.
Alisema timu hiyo ilipeleka vipimo hivyo Mei 15, mwaka
huu kwa ajili ya kubaini aina gani ya ugonjwa, ambapo timu hiyo iliahidi kutoa
majibu mwishoni mwa wiki.
Kwa upande wake Mkuu wa Mkoa aliwataka wananchi
kuwapeleka mapema hospitali watu watakaoonekana na dalili za ugonjwa huo.
MAJIRA
No comments:
Post a Comment