MCHUNGAJI wa Kanisa la Ufufuo na Uzima jijini Mwanza,
Samson Gwajima na Ofisa wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU),
Amin Neigwa, wamevamiwa na majambazi ambao wamewajeruhi vibaya kwa kuwakata
mapanga vichwani.
Tukio hilo lilitokea usiku wa kuamkia jana katika Mtaa wa
Lyila, Kata ya Buhongwa, Wilaya ya Nyamagana, jijini Mwanza.
Akizungumza kwa taabu na gazeti hili akiwa wodini kwenye
Hospitali ya Rufaa ya Bugando (BMC), alikolazwa kwa matibabu, Neigwa, alisema
akiwa sebuleni nyumbani kwake na mkewe, ghafla walimuona msichana wa kazi
aliyekuwa nje akichota maji, akiingia ndani kwa kasi na kukimbilia chumbani.
Alisema wakati akitahamaki kilichotokea, watu
wanaosadikiwa kuwa majambazi waliingia ndani wakiwa na silaha za jadi kama
mapanga, nyundo, vitu vyenye ncha kali na kutaka fedha.
"Walikuwa sita na baadhi yao walifunika sura zao kwa
vitambaa, walinitaka niwape pesa...nilipata ujasiri wa kumrukia mmoja wao
aliyekuwa na panga na kumkaba ndipo wengine wakanishambulia kwa kutumia silaha
zao hadi nikapoteza fahamu," alisema.
Aliongeza kuwa, wakati wanamshambulia wengine walikuwa
wanamlazimisha mkewe awape pesa lakini aliwakatalia na baadaye aliamua kuwapa
sh. 10,000 ambayo ilikuwepo wakaichukua.
"Kelele nilizopiga wakati tumevamiwa zilisikika kwa
majirani ambao walijitokeza ndipo wavamizi wakakimbia," alisema Neigwa
ambaye alijeruhiwa kichwani ambapo hadi jana alikuwa akitokwa na damu
masikioni.
Baada ya watu hao kukimbia, walienda kuvamia nyumbani kwa
Mchungaji Gwajima na kumjeruhi kichwani kwa panga ambapo
hivi sasa amelazwa katika hospitali hiyo kwenye Chumba
cha Wagonjwa Wanaohitaji Uangalizi Maalumu (ICU).
Mchungaji Gwajima ni kaka wa Kiongozi wa Kanisa la Ufufuo
na Uzima, Askofu Josephat Gwajima, ambaye alivamiwa alipokuwa amelala na
familia yake eneo la Lyila na kulazimishwa kutoa fedha.
Akizungumza na gazeti MAJIRA, Mchungaji wa kanisa hilo,
John Kiula, alisema Mchungaji Gwajima
alivamiwa usiku ambapo baadhi ya mashuhuda walidai baadhi ya meno yake
yameng'oka.
"Hadi sasa bado hajajitambua, tumetoka kwenye kipimo
cha CT-Scan lakini majibu bado hatujapewa tumeambiwa yakiwa
tayari watatujulisha," alisema Mchungaji Kiula.
Mkuu wa Idara ya Dharura hospitalini hapo, Dkt. Derick
David, alikiri kuwapokea majeruhi hao usiku na kusema Mchungaji Gwajima
alifikishwa akiwa na hali mbaya zaidi kuliko Neigwa.
"Gwajima ana jeraha kubwa kwenye paji la uso ambalo
ni kama sentimita mbili hadi tatu kwa urefu kwenda ndani, kipimo cha X-Ray
kimeonesha hajapasuka mfupa ila hali yake si nzuri.
"Hadi sasa bado hajitambui, tunatarajia kumfanyia
kipimo kikubwa cha CT-Scan ambacho kitaonyesha ameumia kiasi gani lakini Neigwa
anaendelea vizuri ingawa naye anahitaji kupimwa na CT-Scan ili kuona majeraha
yake kama amepata athari ndani ya kichwa, tunaendelea kuokoa maisha yao,"
alisema.
Kamanda wa Polisi mkoani humo, Naibu Kamishna wa Polisi,
Charles Mkumbo, alikiri kutokea kwa matukio hayo na kuahidi kuyatolea ufafanuzi
ambapo baadhi ya watu wamekamatwa wakihusishwa na matukio hayo.
"Mkuu wa Upelelezi Mkoa na timu yake walikuwa
wanaendelea na uchunguzi, wakiukamilisha nitalizungumzia kwa undani na kuwataja
walioshikiliwa, baadhi ya majambazi hao wametambuliwa na majirani,"
alisema.
No comments:
Post a Comment