Mbunge wa viti maalum Esther Bulaya, CCM |
Mbunge wa Viti Maalum, Ester Bulaya (CCM) (pichani),
ameishambulia Serikali hususani Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa
Mazingira (Nemc) kuwa ndumila kuwili kwa kushindwa kubomoa hekalu lililojengwa
eneo la Mbezi Beach, Dar es Salaam.
Alisema hayo wakati akichangia hotuba ya bajeti ya Ofisi
ya Makamu wa Rais (Mazingira) jana.
Alisema kumekuwa na double standard (undumila kuwili) kwa
serikali kutekeleza matakwa ya kisheria kwa watu waliojenga majumba kama vile
maeneo ya ufukwe wa bahari ambayo hayaruhusiwi kisheria.
Alisema tabia hiyo ya undumila kuwili, imesababisha
kubomolewa kwa nyumba za watu aliowataja kuwa ni dagaa na kuziacha nyumba za
watu wenye nazo ambao ni mapapa.
“Wengine (mapapa) wapo humu ndani, sijui kushoto au kulia
kwangu. Majumba waliyojenga yamesababisha Mto Mbezi kuziba na kupasua daraja
mara kwa mara nyakati za masika,” alisema.
Alisema katika zoezi la bomoamboa lililoendeshwa na Nemc,
nyumba 24 zilibomolewa maelezo kuwa zilijengwa kando ya mito ya Mbezi na
Mndumbwe na eneo la hifadhi ya miti ya mikoko lakini taasisi hiyo imeshindwa
kubomoa hekalu la zaidi ya Sh. Bilioni moja.
“Jumba la Shilingi bilioni moja lile bomoeni…mnasema
sheria ni msumeno, huu msumeno unakata kwa baadhi tu huku kwa wengine unakuwa
butu?,” alihoji.
Alisema ingawa baadhi ya wamiliki wa nyumba hizo kati ya
24 walikwenda mahakamani kupinga nyumba zao zisibomolewe sawa na mmiliki wa
jengo la zaidi ya shilingi bilioni moja, lakini nyumba zao zilibomolewa.
“Msumeno huu unakata kwa wengine tu kwa mapapa unakuwa
butu,” alisisitiza na kuongeza, “hii ni double standard.”
Oktoba mwaka 2012, Waziri Kivuli, Wizara ya Ardhi, Nyumba
na Maendeleo ya Makazi ambaye pia ni Mbunge wa Kawe, Halima Mdee (Chadema),
alisema Serikali inatakiwa kumdhibiti na kumuondoa, kisha kuibomoa nyumba ya
Mbunge wa Viti Maalum (CCM), Mchungaji Getrude Lwakatare.
Alisema wakati
raia wengine wakibomolewa nyumba ambazo kama ilivyo ya Mchungaji Lwakatare,
zilijengwa kinyume cha sheria, Mbunge huyo amehamia na kuishi kwenye nyumba
yake.
Julai mwaka 2012, nyumba za wananchi waliojenga katika
maeneo tengefu ya ufukwe wa Jangwani, Mto Ndumbwi na Mto Mbezi, zilibomolewa
katika operesheni iliyoendeshwa na Nemc.
Hata hivyo, Septemba 2012, Nemc ilithibitisha kukwama kwa
mpango wa kubomoa nyumba hiyo inayokadiriwa kuwa na thamani ya Sh. bilioni 1.5
kutokana na zuio la mahakama.
Mwanasheria wa Nemc, Manchare Heche, alithibitisha kuwapo
kesi iliyofunguliwa na mmiliki wa jumba hilo.
Kesi hiyo imefunguliwa Mahakama Kuu, Kitengo cha Ardhi.
CHANZO NIPASHE
No comments:
Post a Comment