Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Ufundi Dk. Dhukuru Kawambwa |
Migomo ya wanafunzi wa vyuo vikuu iliyoanza juzi
kuishinikiza Bodi ya Mikopo ya Wanafunzi wa Elimu ya Juu (HESLB) kuwalipa fedha
za kujikimu, sasa imesambaa nchi nzima.
Jeshi la Polisi Wilaya ya Temeke jana
lilitumia mabomu ya
machozi kuwatawanya wanafunzi wa Chuo Kikuu Kishiriki cha Elimu (Duce) cha Chuo
Kikuu cha Dar es Salaam waliokuwa wamekusanyika katika eneo la chuo hicho kwa
nia ya kufanya mgomo na maandamano.
Tukio hilo lilitokea jana saa 2.00 asubuhi, baada ya
polisi kufika katika eneo hilo wakiwa na silaha za moto na mabomu ya machozi.
Waziri Mkuu wa Serikali ya Wanafunzi wa chuo hicho,
Bugemwe Melkizedeki, alithibitisha wanafunzi hao kutaka kufanya mgomo.
Hata hivyo, alisema yeye pamoja na viongozi wengine wa
serikali ya wanafunzi wakati mgomo huo ukiandaliwa kufanyika.
Alisema wakati huo yeye na viongozi wenzake walikuwa
benki wakifuatilia malipo hayo.
Melkizedeki alisema hadi kufikia saa 4.00 asubuhi jana,
wanafunzi wote 3,500 walikuwa wameingiziwa fedha hizo, ambazo ni Sh. bilioni
1.3.
Alisema katika
tukio hilo, wanafunzi nane walikamatwa na polisi, ambao walipelekwa katika
kituo cha polisi Chang’ombe kabla ya kuachiwa kwa dhamana.
Miongoni mwa wanafunzi waliokamatwa, ni pamoja na Esau
Meshack, anayesoma Kitivo cha Ualimu, ambaye alisema mgomo huo umeathiri ratiba
nzima ya mtihani.
Alisema wakati mgomo huo unafanyika, alikuwa anaingia
kwenye mtihani ndipo yeye na wenzake walipokamatwa na polisi.
Meshack alisema walifikishwa katika kituo hicho cha
polisi, ambako walipekuliwa, huku wakipigwa virungu, makofi kwenye masikio na
kudhalilishwa kwa kuvuliwa nguo.
Wakati hayo yakijiri, wanafunzi wa Chuo Kikuu cha Sayansi
na Teknolojia cha Mtakatifu Joseph jijini Dar es Salaam, Kitivo cha Ualimu wa
mwaka wa kwanza wa masomo, wamepanga kufanya maandamano leo. Tofauti na wenzao wa Duce, maandamano hayo
yanalenga kushinikiza kufunguliwa kitivo hicho chenye wanafunzi zaidi ya 400
baada ya kufungwa kutokana na kudai fedha za kujikimu.
Mwanafunzi wa Sayansi ya Ualimu wa Hesabu katika chuo
hicho, Mayagi Mustaph, alisema zaidi ya wanafunzi 400 wanashindwa kuingia
darasani kutokana na chuo kufungwa.
Waziri wa Fedha wa Serikali ya Wanafunzi hao, Joseph
Jingu, alipoulizwa kuhusiana na hilo, alisema wao kama serikali ya wanafunzi
waliuomba uongozi wa chuo kukifungua kitivo ili kuruhusu wanafunzi kuendelea na
masomo ifikapo Jumatatu ijayo.
Wanafunzi wa Chuo Kikuu cha Iringa (UoI) jana
waliandamana kuishinikiza HESLB kuwapa fedha hizo, ambazo wanadai
zimecheleweshwa muda mrefu na hivyo kuwafanya waishi katika mazingira magumu.
NIPASHE ilishuhudia wanafunzi hao wakitaka kuandamana
chuoni hapo, huku wakitamka kuwa kama wasingeingiziwa fedha jana, lazima
waandamane kuelekea kwenye ofisi ya mkuu wa mkoa.
Askari wa Jeshi la Polisi walionekana wakirandaranda
maeneo ya chuo, kuanzia saa 2.00 asubuhi hadi saa 6.30 mchana wakiwa na silaha
mbalimbali, yakiwamo maji ya kuwasha, mabomu ya machozi na risasi za moto.
Mkuu wa Wilaya ya Iringa, Anjelina Mabula, aliwataka
wanafunzi hao kutoandamana, kwani suala lao linafuatiliwa kwa karibu na HESLB.
Kuhusu wanafunzi 89 wa Chuo Kikuu cha Ruaha (Rucu)
waliokamatwa na polisi juzi na kushikiliwa katika kituo cha polisi cha wilaya
mkoani humo, Kamanda Mungi alisema wameachiwa kwa dhamana.
Wanafunzi wa Chuo Kikuu cha Dodoma (Udom) wamegoma
kushinikiza serikali kupatiwa fedha hizo pamoja na kulalamika kukatwa fedha
nyingi kwa ajili ya Bima ya Afya.
Mgomo huo ulianza
juzi usiku na kuendelea hadi jana kwa wanafunzi wa Kitivo cha Elimu, Kozi
Maalumu kwa ajili ya walimu wa masomo ya sayansi na hisabati pamoja na Kitivo
cha Sanaa ya Lugha na Sayansi ya Jamii.
Wakizungumza kwa nyakati tofauti mbele ya viongozi
waliotumwa na Waziri Mkuu, Mizengo Pinda, kusikiliza madai yao, wanafunzi hao
walisema wanashindwa kuingia madarasani kutokana na hali ngumu waliyo nayo.
Waziri wa Mikopo wa Serikali ya Wanafunzi katika Kitivo
cha Elimu, Mpandalume Simon, alitaja sababu za mgomo huo kuwa ni kuishinikiza
serikali kusikiliza kilio chao cha kucheleweshewa fedha hizo.
Alitaja madai mengine kuwa ni kukatwa Sh. 100,000, lakini
vyuo vikuu vingine wanalipa Sh. 50,400 kwa ajili ya huduma ya bima ya afya.
Akizungumza na wanafunzi hao, Mkuu wa Mkoa wa Dodoma,
Chiku Galawa, alisema serikali imesikia kilio chao na ndio maana waziri mkuu
aliwatuma kuwasikiliza kutokana na yeye kubanwa na majukumu ya kiserikali bungeni.
“Kabla ya kuonana na nyie tumepita utawala wa chuo na
wamethibitisha juu ya malalamiko yenu na wanasubiri fedha zikishafika,
watahakikisha ifikapo Jumatatu zitakuwa tayari chuo,” alisema Galawa.
Naibu Waziri wa Afya na Ustawi wa Jamii, Stephen Kebwe,
alisema amefika na viongozi wa Mfuko wa Bima ya Afya (NHIF) pamoja na Mganga
Mkuu wa Mkoa wa Dodoma ili kusikiliza malalamiko hayo.
Hata hivyo, baada ya mazungumzo hayo, viongozi hao
walijikuta katika wakati mgumu baada ya kuzomewa na wanafunzi na kulazimika
kukatisha mazungumzo bila kufikia mwafaka wakidai hawawataki, wanamtaka waziri
mkuu mwenyewe.
NIPASHE
No comments:
Post a Comment