Wednesday, May 20, 2015

Kauli ya mama aliyefiwa na watoto wake wawili wakiwa ibada kanisani kwa Askofu Gwajima kwa kinachodaiwa ni shoti ya umeme

Wakati mama mzazi wa watoto wawili waliofariki dunia katika Kanisa la Ufufuo na Uzima, akifunguka kwa kusema kuwa anamwachia Mungu, Askofu wa Kanisa hilo, Josephat Gwajima, amesema tukio hilo ni ajali kama nyingine.
Mama wa watoto hao, Regina Saferi (32), amesema kwa kuwa Mungu ametaka iwe hivyo, hana la kufanya na anamuchia yeye (Mungu).


Kadhalika, Regina amesema kuwa haamini kama vifo vya watoto wake vimesababishwa na utoaji kafara kama baadhi ya watu wanavyodhani, lakini pia haamini kama kweli watoto wake walifariki dunia kwa kupigwa na hitilafu ya umeme.

Akizungumza na NIPASHE jana nyumbani kwake, Mbezi Juu, Dar es Salaam, alisema kuwa kama ni kweli walitolewa kafara, wangefariki dunia na watoto wengine waliokuwapo wakicheza na watoto wake. Alisema anaamini ni shetani aliyetoka nje ya Kanisa na kutenda uovu huo.

Regina alidokeza kuwa siku moja kabla ya kutokea kwa tukio hilo, aliota ndoto ya kutokea kwa msiba, lakini hakujua utatokea wapi na utamfika nani.

“Niliota ndoto, ilikuwa siku ya Jumamosi, niliota watu wengi wamekusanyika katika msiba wakiomboleza, sikujua kama ndoto ile ilikuwa inanihusu mimi na watoto wangu,” alisema Regina akiwa katika hali ya huzuni. Kwa mujibu wa Regina, haamini wala hakukuwa na mazingira ya kutokea kwa hitilafu ya umeme katika eneo hilo.

Alifafanua kuwa baada ya tukio la vifo vya watoto wake Sarah David na Goodluck David, kutokea watoto wengine walikwenda kucheza katika eneo hilo.

Alisema ni miaka minne sasa tangu aanze kusali katika kanisa hilo na hajawahi kusikia wala kuona tukio la kutokea kwa hitilafu ya umeme kanisani hapo.

ASKOFU GWAJIMA
Wakati Regina akisema kuwa anamwachia Mungu, Askofu Gwajima amesema vifo vya watoto hao anavifananisha na tukio la mtu yeyote ambaye atashika nyaya za umeme barabarani na kufariki dunia.

Hata hivyo, Askofu Gwajima hakutoa maelezo zaidi kuhusiana na vifo vya watoto hao. Juzi, Askofu Gwajima alisema alipata taarifa za tukio hilo na alikuwa anafuatilia kuzipata kwa undani.

MIPANGO YA MAZISHI
Baba mzazi wa watoto hao, David Oturo, jana alilieleza NIPASHE kuwa wanasubiri taarifa kutoka Jeshi la Polisi kabla ya kuendelea na mipango ya mazishi.

Oturo alisema kwamba taratibu za uchunguzi wa polisi zikishakamilika, wataisafirisha miili ya watoto wake kwenda mkoani Mara kwa mazishi.

Alisema kuwa Jeshi la Polisi limewaeleza kuwa linaendelea na uchunguzi huo. “Tunasubiri uchunguzi wa Polisi ukamilike, ila ninaamini utakamilika kesho (leo) na kesho (leo) hiyo hiyo jioni tunatarajia kuaga na kesho kutwa (kesho) alfajiri tunatarajia kuanza safari ya kuelekea Musoma,” alisema Oturo.

Alisema viongozi wa Kanisa la Ufufuo na Uzima wanashirikiana nao katika msiba huo, lakini hakutaja ni mchango gani walioupokea hadi sasa kutoka katika kanisa hilo.

SHULE YAMLILIA MWANAFUNZI WAO
Mwalimu wa darasa alilokuwa anasoma marehemu Sarah katika Shule ya Msingi Mirambo jijini Dar es Salaam, Asia Abdallah, ameelezea kuhuzunishwa na kifo cha mwanafunzi wake. Alisema Sarah alikuwa ni mwanafunzi mwenye bidii darasani, hakuwa mtundu na alikuwa anasoma kwa bidii.

Alisema wao kama shule wamepokea kwa huzuni taarifa ya kifo cha mwanafunzi wao na wako bega kwa bega na familia ya marehemu.

“Kitaaluma Sarah alikuwa ni mwanafunzi mzuri, tangu tulipopokea taarifa ya msiba tumehuzunika sana, alikuwa ni mwanafunzi mwenye nidhamu na alikuwa anawahi shuleni,” alisema Abdallah.

KAULI YA POLISI
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kinondoni, Camillius Wambura, alieleza kuwa uchunguzi wa tukio hilo unaendelea.

Alisema Jeshi la Polisi limeshakwenda na wataalam wa umeme kutoka Shirika la Umeme Tanzania (Tanesco) kuangalia na kupima mazingira lilipotokea tukio hilo.

NIPASHE

No comments:

Post a Comment