Mwenyekiti Mtendaji wa IPP, Dk. Reginald Mengi, ameeleza
kusikitishwa dhidi ya majibu yaliyotolewa na Kurugenzi ya Mawasiliano ya Rais
Ikulu kuhusu taarifa za kamchafua zilizochapishwa na gazeti la Taifa Imara
Machi 20, mwaka huu.
Dk. Mengi, alisema
jana kuwa majibu yaliyotolewa na
Mkurugenzi wa Kurugenzi hiyo, Salva Rweyemamu, siyo ya busara kwani yanapuuza
usalama wa maisha yake.
“Majibu haya ya Salva yanaongeza hofu ya usalama wa
maisha yangu jambo ambalo siyo dogo na la kupuuzwa kama anavyoona yeye,”
alisema Dk. Mengi na kuongeza:
“Ukiangalia, ukisoma kiundani majibu ya barua ya
Rweyemamu, nina kila sababu ya kuhofia usalama wa maisha yangu. Shughuli zake
Ikulu ni za kuheshimiwa, lakini awe na busara katika shughuli zake….kunishauri
eti niende polisi kuhusu suala hilo ni kama kunifanya nionekane sina busara
kama yeye.”
Alisema uhai wa mtu siyo jambo dogo wala siyo la kupuuzwa
na kwamba busara ilihitajika katika kushughulikia suala hilo, lakini haikuwa
hivyo kwani majibu hayo yamesababisha tatizo hilo dhidi ya usalama wa maisha
yake kuwa pale pale.
Machi 23, mwaka huu, gazeti la Taifa Imara, lilichapisha
habari iliyoeleza kuwa, Kiongozi Mkuu wa ACT Wazalendo, Zitto Kabwe,
alimchongea Dk. Mengi kwa Rais Kikwete, kwamba ndiye kinara wa kuihujumu
serikali yake na alikuwa anamshawishi Zitto kujiunga na mipango hiyo.
Habari hiyo
iliendelea kudai kuwa, Dk. Mengi aliapa kumshughulikia Rais Kikwete kwa nguvu
zake zote amalizapo muda wake wa urais huku Rais Kikwete naye akiapa kupambana
na yeye (Dk. Mengi).
Aprili 17 mwaka huu, katika mkutano wake na waandishi wa
habari, Dk. Mengi alisema, tuhuma hizo
dhidi yake zilimshtua sana na kumpa hofu kubwa kwa usalama wa maisha yake hivyo
kuilaumu kurugenzi ya mawasiliano Ikulu
na Idara ya Habari (Maelezo) kwa kukaa kimya zaidi ya wiki tatu bila
kutoa ufafanuzi wowote kuhusu habari hiyo ambayo pia inamhusu Rais na kuiacha
kusambaa.
“Nilitoa kauli kwamba, tuhuma hizo dhidi yangu
zilinishtua sana na kwamba tamko la Mheshimiwa Rais kwamba atapambana nami
lilinipa hofu kubwa kuhusu usalama wa maisha yangu,” alisema Dk. Mengi.
Dk. Mengi alisema
majibu yaliyotolewa na kurugenzi ya Mawasiliano ya Rais Ikulu, yalieleza kuwa
Rais hakuwahi kuwa na mawasiliano na Zitto Kabwe kama ilivyoelezwa na kwamba
haikufanya lolote kutokana na kubanwa na majukumu, hivyo kupuuza habari hizo
kwa kuziona ni ndogo na za upuuzi.
“Salva hakufanya lolote eti kutokana na kuwa na majukumu
mengi na alipuuza habari hizo kwa sababu aliziona ni jambo dogo na upuuzi,”
alifafanua Dk. Mengi na kuongeza:
“Bwana Rweyemamu alisema pia kwamba alinishangaa kwa kutokutoa
taarifa katika kituo chochote cha Polisi kuhusu hofu ya usalama wa maisha
yangu. Majibu haya ya Salva yanaongeza hofu ya usalama wa maisha yangu, jambo
ambalo siyo dogo na la kupuuzwa kama anavyoona yeye.”
CHANZO: NIPASHE
No comments:
Post a Comment