Friday, May 22, 2015

VIKAO VIZITO VYA CCM KUANZA LEO....Ajenda muhimu katika mikutano hiyo ni ratiba ya uchaguzi pamoja na kuwapata wagombea wa chama hicho ngazi zote.

CHAMA Cha Mapinduzi (CCM) kimejigamba kitatoka katika vikao vyake muhimu vya Kamati Kuu (CCM) na Halmashauri Kuu ya Taifa (NEC) vinavyoanza mjini hapa leo kikiwa imara kuliko hapo awali.

Kauli hiyo imetolewa na Katibu wa Itikadi na Uenezi Chama cha Mapinduzi (CCM) Taifa, Nape Nnauye wakati akijibu swali kuhusiana na vikao vizito vya chama hicho vinavyoanza leo.

Nnauye alikuwa anaelezea maandalizi ya vikao vya kamati kuu kinachotarajia kuanza leo na halmashauri kuu ambayo itaanza kikao chake cha siku mbili kesho. Katibu huyo amesema
wajumbe wa vikao hivyo ambavyo vitatoa mwelekeo wa sura ya uchaguzi itakavyokuwa ndani na nje ya chama hicho wameshaanza kuwasili mjini hapa.

Ajenda muhimu katika mikutano hiyo ni ratiba ya uchaguzi pamoja na kuwapata wagombea wa chama hicho ngazi zote. Ajenda nyingine ni hali ya kisiasa nchini na kutolewa kwa ratiba ya uchaguzi.

Pia vikao hivyo vinatarajia kutoa ratiba ya mchakato wa uchaguzi wa Urais na wagombea wengine, kutengeneza kanuni za kuwapata wagombea. Mambo mengine ni kupanga tarehe ya kuchukua fomu, kuzunguka kutafuta wadhamini na masuala mengine ambayo yanakigusa chama.

Mambo yanayotarajiwa kujadiliwa katika vikao hivyo ni pamoja na hatma ya makada wanaotaka kuwania kiti cha Urais ambao walitangaza nia kabla ya wakati na wakatolewa karipio na chama hicho cha kuwataka watulie na kusubiri muda mwafaka.

Tayari kamati ndogo ya Udhibiti na Nidhamu ya CCM chini ya Mwenyekiti wake, Philip Mangula ambaye pia ni Makamu Mwenyekiti wa CCM -Taifa, imeshafanya vikao vyake mjini Dodoma kupitia taarifa za utekelezaji wa adhabu kwa makada sita wa chama hicho wanaodaiwa kuanza kampeni kuwania urais mwaka 2015 kabla ya wakati.

Makada hao waliozuiwa kujihusisha na kampeni kwa miezi 12, huku mienendo yao ya kisiasa ikifuatiliwa ni January Makamba, Waziri Mkuu wa zamani, Edward Lowassa na Waziri Mkuu mstaafu, Frederick Sumaye.

Wengine ni Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Bernard Membe, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais (Uhusiano na Uratibu), Steven Wassira na aliyewahi kuwa Waziri wa Nishati na Madini ambaye ni Mbunge wa Sengerema, William Ngeleja.

HABARI LEO

No comments:

Post a Comment