Ilikuwa ni kama kutekeleza maandiko ya Biblia yanayosema
“jifungeni nguo za magunia, ombolezeni na kulia kwa uchungu”, wakati ndugu
walipokwenda Hospitali ya Rufaa ya KCMC kuchukua mwili wa marehemu.
Walikuwa wamevalia magunia,
lakini sababu ya kuvalia nguo
hizo haikuwa kama maandiko hayo yanavyosema kuwa “kwa sababu hiyo jifungeni
nguo za magunia; ombolezeni na kulia kwa uchungu; kwa maana hasira kali ya
Bwana haikugeuka na kutuacha”.
“Tumejiuliza maswali mengi, tumeshindwa kupata majibu.
Tumejiuliza tuvae nguo gani hatukupata majibu. Kwa kuvaa hivi tunataka hao
wauaji wajue damu hii itawalilia popote walipo,” alisema Beata Kiria, ambaye ni
dada wa Victoria Sylvester aliyeuawa na watu wasiojulikana na mwili wake
kuzikwa nusu kiwiliwili.
Beata na ndugu zake walifika kwenye hospitali hiyo kwa
ajili ya kuuchukua mwili huo wakiwa wamevalia magunia.
Tukio hilo lilitokea jana kati ya saa 4:30 asubuhi na saa
6:00 mchana wakati ndugu hao walipofika chumba cha kuhifadhi maiti cha
hospitali, huku baadhi yao wakiwa pekupeku na kusababisha watu wengi waliokuwa
eneo hilo pamoja na watumishi wa hospitali kuwashangaa.
Wakiwa ndani ya chumba cha kuhifadhia maiti, ndugu hao
walilia wakipaza sauti wakitaka wauaji wa mwanamke huyo wakamatwe kabla ya
kuchukua mwili na kuondoka nao.
Victoria (53), mkazi wa Kijiji cha Masherini, Umbwe eneo
la Kibosho aliuawa kwa kukatwa mapanga usiku wa kuamkia Ijumaa iliyopita na
baadaye wauaji kuuzika mwili wake nusu na kuacha kiwiliwili nje ya nyumba
waliyokuwa wakiishi, jambo lililoibua utata mkubwa ndani ya familia hiyo.
Akizungumza na gazeti hili, Kiria alisema walichagua
mavazi hayo baada ya kukosa vazi lingine.
“Tulitafakari tuvae nguo gani ili kumuenzi marehemu
lakini hatukupata jibu, ndiyo tukaamua tuvae magunia kuonyesha kuwa waliomuua
ndugu yetu thamani yao inafanana na magunia haya,” alisema Kiria.
Imezoeleka misiba mingi ndugu huvaa suti nyeusi kwa
wanaume huku wanawake wakivalia mavazi meusi au meupe ambayo baadaye hujifunika
na vitambaa vyeusi au vyeupe kwa akina mama.
Kiria, ambaye alizungumza kwa niaba ya familia, alilitaka
Jeshi la Polisi kuhakikisha linawatafuta na kuwakamata watu waliohusika na
mauaji hayo.
Kamanda wa polisi mkoani Kilimanjaro, Fulgence Ngonyani
alisema wanamshikilia mume wa marehemu, Silvester Mmasi na mtumishi wao ambaye
hakumtaja kwa ajili ya mahojiano kuhusu mauaji hayo na polisi inaendelea
kuwatafuta washukiwa wengine.
MWANANCHI
No comments:
Post a Comment