Tuesday, May 19, 2015

WATOTO WA VIGOGO BOT WANA KESI YA KUJIBU.....NI KATIKA TUHUMA ZA KUGHUSHI VYETI..

Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu imewaona wafanyakazi wanane wa Benki Kuu ya Tanzania (BoT) wanaokabiliwa na tuhuma za kughushi vyeti na kutoa hati za uongo wana kesi ya kujibu.

Uamuzi huo ulitolewa jana
na Hakimu Mkazi, Nyigulile Mwaseba baada ya kupitia ushahidi uliotolewa na mashahidi wanane wa upande wa mashtaka pamoja na vielelezo vilivyowasilishwa mahakamani hapo.

Baada ya Hakimu Mwaseba kutoa uamuzi huo, alisema Juni 17 na 18, 2015, washtakiwa hao ambao wanadaiwa kuwa ni watoto wa vigogo wa Serikali wataanza kutoa ushahidi wa utetezi dhidi ya mashtaka yanayowakabili.

Wafanyakazi hao ni Justina Mungai, Christina Ntemi, Siamini Kombakono, Janeth Mahenge, Beatha Massawe, Jacquiline Juma, Philimina Mutagurwa na Amina Mwinchumu.

Washtakiwa hao kwa pamoja wanadaiwa kughushi vyeti vya kuhitimu kidato cha nne na kutoa hati za uongo kwa mwajiri wao, BoT.

Washtakiwa Mungai, Massawe na Mwinchumu, wanadaiwa kughushi vyeti hivyo mwaka 2001, wakati Ntemi, Kombakono, Mahenge na Mutagurwa wanadaiwa kughushi vyeti hivyo mwaka 2002.

Wanadaiwa kughushi vyeti vya kuhitimu kidato cha nne na kutoa BoT hati za uongo wakionyesha kuwa vimetolewa na Baraza la Mitihani la Taifa wakati siyo kweli. Washtakiwa hao ambao awali waliyakana mashtaka, wako nje kwa dhamana.

MWANANCHI

No comments:

Post a Comment