Watoto wawili ambao ni ndugu, wamefariki dunia katika
Kanisa la Ufufuo na Uzima, linaloongozwa na Askofu Josephat Gwajima, jijini Dar
es Salaam.
Watoto hao walifariki dunia kutokana
na kupigwa na shoti
ya umeme wakiwa katika ibada juzi.
Tukio hilo lilitokea wakati watoto hao wakiwa na waumini
wengine wakifuatilia ibada ya kufunga ndoa.
Inadaiwa kuwa, watoto hao walipigwa na shoti baada ya
kukanyaga nyaya za umeme wakati wao na waumini wengine walipoamka vitini kwenda
kuwapokea maharusi wakati wakiingia kanisani hapo.
BABA ATILIA SHAKA
Hata hivyo, baba mzazi wa watoto hao, David Oturo,
ameonyesha hali ya wasiwasi na kutokukubalina na mazingira ya vifo vya watoto
wake, Sarah (10), Goodluck (4) na kusema ni vifo vya utatanishi.
Akizungumza na NIPASHE jana kuhusiana na vifo hivyo
alieleza kuwa, Sarah alikuwa anasoma Shule ya Msingi Milambo iliyopo Mbezi Juu
darasa la nne na Goodluck alikuwa anasoma chekechea ya Ushindi.
Alisema siku hiyo kulikuwapo na watoto wengi
waliokusanyika katika viwanja vya kanisa hilo, lakini ni watoto wake tu ndiyo
waliofikwa na mauti huo.
“Pale kanisani kulikuwa na watoto wengi na waumini
wengine lakini kwanini imetokea kwa watoto wangu tu?” alihoji.
Aliongeza kuwa kabla ya kukutwa na mauti jioni, majira ya
mchana, Sarah aling’atwa na nyuki sehemu ya mguuni waliotokea katika kanisa hilo
ghafla.
Alisema ilipofika jioni ndipo watoto wake peke yao
walikanyaga nyaya za umeme zilizokuwa zimepitishwa katika viwanja hivyo.
Oturo alifafanua kuwa nyanya hizo za umeme hazikuwa
zimechunika wala hazikuwa na dalili ya kuwa na hitilafu.
“Sehemu yenyewe haikuwa na mchubuko wowote wa waya, wala
hakukuwa na hitilafu yoyote, ilikuwa ni sehemu ambayo inaonekana imetengenezwa
na mtu ambaye ni mtaalam wa masuala ya umeme,” alisema Oturo.
Alisema watoto hao walikuwa na mama yao ambaye ndiye anayekweda
nao kila siku ya Jumapili katika ibada.
Oturo aliongeza kuwa, baada ya watoto wake kupigwa na
shoti ya umeme, walipewa huduma ya kwanza na uongozi wa kanisa hilo na kisha
kukimbizwa katika Hospitali ya TMJ.
Akielezea huku akionekana kuwa na huzuni, Oturo alisema
baada ya kufikishwa katika hospitali hiyo, walipelekwa katika hospitali ya
Mwananyamala na ndiko mauti yalipowafikia.
“Sehemu yoyote kunapokuwa na shoti lazima fundi umeme
atakuwapo, lakini kitu cha kushangaza kwa nini imewakuta watoto wangu tu,
wakati kulikuwapo na umati wa watu wengi?” alihoji baba wa watoto hao.
Alisema waliripoti tukio hilo katika Kituo cha Polisi cha
Kawe na kuandikiwa RB KW/RB/5374/2015.
Oturo alisema kwa sasa wanasubiri uchunguzi wa Jeshi la
Polisi ili miili isafirishwe kuelekea Musoma, mkoani Mara kwa mazishi.
MASHUHUDA WASIMULIA
Baadhi ya mashuhuda waliokuwapo wakati wa tukio hilo, Aida Simon na Sylvia Gozbert,
walieleza kuwa siku ya tukio kulikuwa na harusi kanisani hapo.
Walisema maharusi walipokuwa wanaingia kanisani, Askofu
akawaambia watoto na waumini kwenda kuwapokea na kuwashangilia maharusi hao.
Walisema ghafla wakati tukio hilo likiendelea ndipo
watoto hao walipigwa na shoti ya umeme.
UONGOZI WA KANISA WAZUNGUMZA
Askofu wa Kanisa hilo, Josephat Gwajima, alisema kuwa
tukio hilo lilitokea baada ya yeye kuondoka kanisani hapo.
Alisema ni kweli watoto hao walifariki kutokana na shoti
ya umeme iliyotokea kanisani hapo.
“Kwa sasa sina taarifa kamili kwa sababu tukio lilitokea
baada ya mimi kuondoka kanisani, lakini ni kweli watoto hao wamefariki na hivi
sasa ninaelekea kanisani ambako nitapata taarifa kamili,” alisema Gwajima.
KAULI YA POLISI
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kinondoni, Camillius Wambura,
alithibitisha kutokea kwa tukio hilo. Wambura alilieleza NIPASHE kuwa, uchunguzi bado unaendelea wa kubaini kama ni
kweli tukio hilo lilisababishwa na kukanyaga nyaya za umeme.
Alisema polisi pia wanachunguza kufahamu kama kuna tukio la makusudi ama kulikuwa na uzembe wowote uliosababisha
kutokea kwa vifo hivyo.
“Baada ya uchunguzi huo kukamilika, ndipo tutajua ni
hatua gani za kisheria tutakazozichukua kutokana na tukio hilo,” alisema
Wambura.
CHANZO: NIPASHE
No comments:
Post a Comment