JESHI la Polisi Mkoa wa Morogoro linamshikilia mwanafunzi
wa kidato cha kwanza katika Shule ya Sekondari Kolla Hill, Judith Chomile (15)
kwa tuhuma za mauaji.
Mwanafunzi huyo anadaiwa kumnyonga ndugu yake, Edrin
Mafwele (9) ambaye ni mwanafunzi wa Shule ya Msingi Benard Bendel iliyopo
Manispaa ya Morogoro.
Tukio hilo lilitokea juzi usiku wakati watoto hao
walipokuwa nyumbani kwao.
Baba wa marehemu Edrin Mafwere aliyefahamika kwa jina la
Barnabas Mafwele, mkazi wa eneo la Kola, alisema jana kuwa mtoto wake
alinyongewa chumbani.
“Kabla ya kifo hiki, Mei 10 mwaka huu, majira ya usiku,
mwanangu Edrin alipiga kelele na kusema kuna mtu alikuwa ameficha uso wake kwa
kitambaa akitaka kumkaba shingo.
“Wakati anapiga kelele sisi tulikuwa sebuleni na
tulipomuuliza mtu huyo yukoje alisema anafanana na dada yake Judis ambaye ni
mtoto wa ndugu yangu.
“Baada ya muda kidogo tulimuona Judith akiingia ndani na
tulipomuuliza alikuwa wapi alisema alikuwa amekwenda dukani.
“Baada ya tukio hilo niliwahoji watoto hao na baadaye
nikawaacha na leo mtoto wangu amefariki dunia kwa kunyongwa.
“Ingawa hakuna ushahidi wa moja kwa moja wa nani
alimnyonga mtoto huyo, hapa nyumbani tumepata khanga iliyotapakaa damu,
tumepata kitanzi kilichotengenezwa kwa nguo na vitu vyote hivyo ni vya hapa
hapa nyumbani kwangu,” alisema Mafwele.
Wakati mzazi huyo akisema hayo, Kamanda wa Polisi, Mkoa
wa Morogoro, Benald Paul, alisema taarifa alizozipata zinaonyesha mtoto huyo
alifariki dunia baada ya kuanguka ghafla alipokuwa sebuleni.
“Taarifa zetu zinasema mtoto huyo alianguka ghafla akiwa
sebuleni na alipopelekwa katika hospitali ya mkoa iligundulika kuwa alikuwa
amekwisha kufariki dunia.
“Hata mtuhumiwa Judith tulipomhoji, alituambia marehemu
alianguka na kutokwa damu puani pamoja na mkojo baada ya kupoteza fahamu.
“Hata hivyo, bado tunaendelea kumshikilia mtuhumiwa huyo
kwa ajili ya kupata uhakika zaidi wa tukio hilo,” alisema Kamanda Paul.
MTANZANIA
No comments:
Post a Comment