MOJA ya mambo ambayo yamekuwa yakisumbua vichwa vya
wanajamii walio wengi, ni kutambia misaada tunayopewa na nchi wahisani na madai
kuwa tunakubalika au nchi hizo zinaikubali nchi yetu kwa kutupa misaada.
Kinachosumbua zaidi ni kwamba, misaada inayotolewa walio
wengi
huwa hawajui inatumika vipi na wengine wanaweza kusema kuwa hawajaona
faida ya misaada yenyewe.
Mara nyingine misaada hiyo inaweza kuwa ni ya kutupambaza
licha ya tambo kuwa tuna rasilimali nyingi ambazo tukizitumia ipasavyo tutapiga
hatua mbele.
Lakini tumekuwa tunasahau jinsi ambavyo tunawaita wageni
kutoka nje kwa madai kuwa zipo fursa za uwekezaji ambazo tunaingia ubia na
kushuhudia mgawanyo ukiwa ni mdogo kwa wenye mali.
Ndani ya mazingira kama hayo, masharti ya misaada
inawekwa na kwa kuwa tunakuwa tumeshalemazwa na misaada inafikia hatua ya
kuyatii masharti hayo ili kuendelea kukubalika kwa wahisani.
Haishangazi kuona kuwa wahisani hao wanatulemaza hata
kwenye mambo yaliyo ndani ya uwezo wetu hasa pale inapotokea wahisani
wanapotujengea hata matundu ya vyoo na baadaye kuwekwa bango ‘kimejengwa kwa
hisani’ ya watu wa nchi husika. Hoja ni kwamba hata yale tunayoyaweza tunaona
ni sifa kusaidiwa?
Hapa inajiweka wazi kwamba tulishasahau ile kampeni ya
‘Mtu ni Afya’ ambayo ilirindima miaka ya 1970 chini ya uongozi wa Baba wa Taifa
Mwalimu Julius Kambarage Nyerere.
Kwa maana hiyo ni kwamba, baada ya kuzama kwenye ‘Mtu ni
Pesa’ basi tukawa tumetawaliwa na mali, tamaa na utengano vyote vikiwa vinaota
mizizi na matunda yake yamekuwa kukosekana kwa uadilifu ambako kumeikumba jamii
leo ikizongwa na ukosefu wa misingi ya uadilifu, uaminifu na ustaarabu na
badala yake kujengeka vitendo vya rushwa, ufisadi na uroho wa madaraka.
Kwa kuzama kwenye lundo hilo, kila uchwao inakuwa ni
kupokea masharti, na hata hivyo wakati huu yanapofanyika maandalizi ya kuandika
Katiba Mpya ni wakati sawia kuwa na kipengele kinachotaja, “Tanzania haitakubali
au kupokea misaada yoyote yenye nia na masharti ya kuondoa au kudhalilisha utu
wetu, utamaduni wetu, utaifa wetu, uhuru wetu na amani yetu.”
Aidha, kipengele hicho kifafanue kwamba nchi yetu
haitapokea misaada yoyote yenye makusudi, masharti au nia ya kutudhalilisha utu
wetu, utaifa wetu, utamaduni wetu, mshikamano wetu, uhuru wetu na yoyote yenye
nia ya kuathiri amani yetu hata kama misaada hiyo ina faida kiasi gani.
Kimsingi uhai wa taifa unategemea nguvu kazi ya vijana na
ambao wengi leo hii wanashuhudia mabadiliko na kasi ya utandawazi yanavyofanya
mabadiliko hayo kuingia ndani ya jamii hata pale, ambapo yanakuwa si kwa hiari,
lakini kwa misingi ya kushinikizwa na wahisani.
Kwa kuona mbali na kutambua hali hiyo, Mwalimu Nyerere
aliweka bayana kwenye moja ya hotuba zake mwaka 1985 aliposema, “Tunataka kuona
katika taifa hili vijana jeuri na wenye kujiamini; si vijana waoga akina ndiyo
bwana.
“Tunataka vijana wenye ujasiri wa kuhoji na kupiga vita
mifumo ya kijamii isiyoshabihiana na matakwa na matarajio ya jamii ya
Kitanzania. Tunataka vijana waasi dhidi ya mifumo kandamizi ya kutugawa na
kuutenga umoja wetu, vijana wenye maadili nidhamu na wasema kweli hata
wakichukiwa.”
Nchi maskini ni wapokeaji wa mambo kuanzia mifumo ya
uchumi, teknolojia na hata tamaduni, hivyo kuingia kwenye mashinikizo kutokana
na kuwa tegemezi kwa misaada.
Mwaka 2011, Waziri Mkuu wa Uingereza, David Cameroon
kwenye Mkutano wa Nchi za Jumuia ya Madola alisema kuwa misaada ya nchi hiyo
haitatolewa kwa nchi zisizozingatia haki za mashoga na wasagaji.
Kauli hiyo iliwachefua viongozi wengi wa nchi za Afrika
ambao wanaunda sehemu kubwa ya wanachama wa jumuia hiyo awali zikitawaliwa na
Uingereza.
Kwa upande wa Tanzania, Waziri wa Mambo ya Nje na
Ushirikiano wa Kimataifa, Bernard Membe, alitoa kauli kuwa ni bora kufa njaa
kuliko kukubaliana na suala la ushoga.
Marekani nayo iliibuka na suala hilo na kutangaza
hadharani kuwa itapambana na ubaguzi wa wapenzi wa jinsia moja nchi za nje kwa
kutumia misaada ili kushinikiza mabadiliko.
Hivyo Tanzania inapinga kwa nguvu zote uhusiano wa
kimapenzi wa jinsia moja. Lakini ni miongoni mwa nchi zinazopokea msaada kwa
wingi kutoka Marekani na Uingereza.
Kati ya nchi zinazopokea misaada na ambayo imepitisha
sheria ya kupingana na matakwa ya nchi za magharibi ni Uganda ambayo inaweza
kuonekana kuwa inamweka Rais Yoweri Museveni katika kitanzi cha kunyimwa
misaada. Lakini mwenyewe alisema kuwa nchi hiyo inaweza kusimama bila msaada
kwani ina utajiri mwingi.
Mashinikizo ya nchi za magharibi yasiyo na tija kwa jamii
yanaweza kubainishwa kwenye historia kwamba chenye udhia kwao, wanataka kiwe
udhia kwa wengine pia.
Walipopiga marufuku mila na tamaduni zetu na hata
kuangusha mifumo ya utawala wakiona kuwa haifai lengo lilikuwa ni kuilisha
jamii utamaduni wao na walifanikiwa.
Udhia huo unawekwa wazi na Mwanahistoria maarufu wa
Ghana, Profesa Adu Boahen kwenye kitabu cha ‘Topics History of West Africa’
anasema kuwa baada ya kutengwa maeneo ya Sierra Leone na Liberia kwa ajili ya
makazi ya watu walioondolewa kwenye utumwa, ndani yake walijumuishwa makahaba
wa Ulaya ambao hawakutakiwa huko kwao.
Hao walionekana kuwa ni udhia kimaadili basi suluhisho
lilikuwa ni kuwapeleka mbali, na hivyo walihamishiwa Sierra Leone.
Mwangwi wa hilo tukio ndio huu kwamba, kwa kuwa udhia huo
umeshaenea miongoni mwa nchi zilizoendelea hivyo kila wanachokiona kukubalika
kwao wanataka kikubalike au kienee sehemu nyingine zisizo na utamaduni huo
hususani Afrika.
Aidha, ili kufanikisha azma ni pamoja na kushinikiza kwa
kutumia udhaifu uliomo ndani ya nchi hizo maskini.
Hiyo inamaanisha kuwa kama shinikizo hilo likikubalika na
kutambuliwa basi itakuwa imefikia hatua nzuri kwao ya kuhamisha udhia wa ushoga
uliomo miongoni mwao na kuuingiza Afrika.
Hata hivyo, kama ni kusimama kidete na kusimamia maadili
kama alivyosema Mwalimu Nyerere wa kuwa na jamii yenye maasi dhidi ya mifumo
kandamizi, basi itakuwa heri umaskini kuliko misaada ya udhalilishaji.
Lakini kwa upande mwingine kauli ya Rais Museveni
inasadifu hapa kwamba tunaweza kusimama wenyewe kwani tuna utajiri mwingi.
JAMBO LEO
No comments:
Post a Comment