Safari ya mbunge wa zamani wa Kigoma Kaskazini kwa tiketi
ya Chadema, Zitto Kabwe kurejea bungeni imeanza rasmi baada ya kiongozi huyo wa
chama kipya cha ACT-Wazalendo kuchukua fomu za kuwania kuongoza jimbo la Kigoma
Mjini.
Uamuzi huo wa kulitaka jimbo
hilo unathibitisha kauli
zake ambazo amekuwa akizitoa kwa muda mrefu kuwa hatarudi tena Kigoma Kaskazini
kwa kuwa alishawatimizia kila kitu na haoni sababu za kuwawakilisha tena
wananchi wa eneo hilo.
Kauli yake iliibua ubashiri kuwa Zitto anataka kubadilishana
jimbo na mbunge wa Kigoma Mjini (CCM), Peter Serukamba, uvumi ambao aliukanusha
akisema hadhani kama CCM inaweza kupata jimbo Kigoma.
Zitto, ambaye alijiondoa Chadema baada ya kukiuka katiba
kwa kufungua mashtaka dhidi ya chama hicho, hakufanya mbwembwe wakati akienda
kuchukua fomu kwenye ofisi za ACT Ujiji jana, badala yake aliita viongozi wa
kata na matawi bila ya kutaarifu vyombo vya habari.
“Nimeamua kugombea ubunge wa Kigoma Mjini ili niwatumikie
ndugu zangu ambao wamekuwa wakipata tabu katika kupigania haki zao za msingi
ambazo walistahili kuzipata kama ilivyo katika mikoa mingine,” alisema Zitto
alipoongea na mwandishi wa Mwananchi kwa simu.
“Nitakapokuwa mbunge wa Kigoma Mjini nitahakikisha
barabara za mitaani zinapitika katika kipindi chote cha mwaka, nitahakikisha
watu wanaacha tabia ya kulima mashamba katikati ya mitaa na makazi, lakini
nitahakikisha kila mmoja anajiunga na mifuko ya kijamii ili kujiwekea akiba ya
uzeeni pamoja na kupata huduma ya matibabu, elimu na nyinginezo zinazopatikana
kwa kutumia mifuko hiyo.”
Mwenyekiti huyo wa zamani wa Kamati ya Bunge ya Hesabu za
Serikali (PAC), alisema bonde la Mto Luiche bado halijatumika ipasavyo
kuzalisha chakula kwa wingi.
“Nakusudia kuibana Serikali ijenge skimu ya umwagiliaji
maji ili wakulima walime kilimo cha mpunga kwa mwaka mzima bila kupumzika,
jambo ambalo litainua uchumi wa wakulima na kuongeza chakula hapa Kigoma,”
alisema.
Kuhusu umeme wa gridi ya Taifa, Zitto alisema lazima
upatikane ili kusaidia jitihada ya ujenzi wa viwanda vya kusindika mazao ya
uvuvi na kilimo kwa kuwa hivi sasa mji wa Kigoma Ujiji unategemea umeme wa
jenereta ambao hauwezi kuendesha shughuli za viwanda, hali inayochangia mkoa
kuendelea kuwa masikini licha ya kuzungukwa na rasilimali nyingi.
Katibu wa ACT wa Jimbo la Kigoma Mjini, Azizi Ally
alisema Zitto alichukua fomu hiyo jana kwa malipo ya Sh100,000 mbele ya
viongozi 72 wa kata na matawi kutoka jimboni humo.
“Kwa hali ya sasa Kigoma Mjini inahitaji kupata mbunge
anayeweza kufuatilia mambo kwa kina ili kuleta maendeleo ya wananchi baadala ya
yule anayekwenda bungeni kujifunza,” alisema Ally.
AFRICANJAM
No comments:
Post a Comment