Polisi wilayani Kahama mkoani Shinyanga, imewakamata watu
watano wanaotuhumiwa kukutwa na viungo vya mtu mwenye ulemavu wa ngozi
(albino), wakiwa katika harakati za kuviuza.
Akizungumza
na NIPASHE jana, Mkuu wa kituo cha polisi
wilayani Kahama, Leonard Nyandahu, alisema watu hao walikamatwa saa 7 mchana
jana katika nyumba ya kulala wageni iitwayo Maji Hoteli, iliyopo Phantom, kata
ya Nyasubi, wilayani Kahama.
Aidha, Kamanda wa Polisi mkoa wa Shinyanga, Justus
Kamugisha, aliwataja watuhumiwa hao kuwa ni Bahati Kirungu (56), ambaye ni
mwalimu wa Shule ya Msingi Katungulu kata ya Wendele, Mhoja John (24), wa
Isagehe-Nzega na Bilia Busanda (39), mkazi wa Mogwa Nzega.
Wengine ni Shija Makandi (60) wa Isagehe-Nzega, Regina
Kashinje (40) wa Isagehe-Nzega na Aboubakary Ally (25) ambaye alikuwa msiri wa
kutafuta wateja, mkazi wa Isagehe- Nzega.
Kamugisha alisema Mei 19, mwaka huu asubuhi, mkuu wa
upelelezi wa kituo cha polisi Nzega, alipata taarifa za mtu akitafuta wateja wa
kununua viungo vya albino, walipoweka mtego walishindwa kumkamata na kuhamishia
biashara yake wilayani Kahama.
Aidha, alisema maafisa upepelezi mkoa wa Tabora kwa
kushirikiana na wale wa Kahama, walifuatilia nyendo za watu hao na kuweka mtego
wa kuwakamata watu hao uliofanikisha kuwanasa.
Alisema jeshi la polisi wilayani Kahama, linaendelea
kuwashikilia watu hao kwa mahojiano zaidi ikiwa ni pamoja na kuubaini mtandao
wao pamoja na kuchukuliwa hatua kali za kisheria.
Kamanda Kamugisha, alisema serikali na jeshi la polisi
itaendelea kuwasaka wauaji wa walemavu wa ngozi na kuhakikisha suala hilo
linamalizwa katika mkoa wa Shinyanga.
No comments:
Post a Comment