Watu wawili, mke na mume wakazi wa Makambo, wilayani Mlele, wameuawa kikatili
kwa kuchinjwa na kutenganishwa kichwa na kiwiliwili wakati wakiwa wamelala.
Kidavashari aliwaambia waandishi wa habari kuwa tukio
hilo lilitokea Mei 21, usiku nyumbani kwa wanandoa hao ambao baada ya kuuawa
miili yao iliachwa kitandani.
Alisema marehemu hao wakati wa uhai wao walikuwa wakiishi
kwenye nyumba yao peke yao kwa muda mrefu.
Alisema, balozi wa
eneo hilo, Wilbroad Mahenge, ndiye aliyegundua vifo hivyo baada ya kutowaona
wanandoa hao kwa siku mbili mfululizo na kuingiwa na wasiwasi.
Kamanda Kidavashari alisema balozi huyo aliamua kwenda
kwenye nyumba ya wanandoa hao ili kujua hali zao na alipofika alikuta milango ikiwa wazi hali iliyosababisha apate
mashaka.
Alisema alijaribu kuwaita kwa majina yao lakini hakuna
aliyeitika na aliamua kuingia ndani na kuwakuta wakiwa wamelazwa kitandani huku
wakiwa wamefariki dunia kwa kuchinjwa shingo zao na kutenganishwa kiwiliwili na
kichwa.
Alisema, balozi Wilbroad alikwenda kutoa taarifa kwenye
uongozi wa serikali ya kitongoji ambao nao walitoa taarifa polisi.
Kamanda alisema chanzo cha mauaji hayo ni imani za
kishirikina.
Aidha, alisema mpaka sasa hakuna mtu aliyekamatwa
kuhusiana na tukio hilo.
Alisema polisi kwa kushirikiana na uongozi na wanakijiji
wa Makambo, wanaendelea na msako ili kuwabaini watu waliohusika katika mauaji
hayo.
NIPASHE
No comments:
Post a Comment