Kwa wafuatiliaji wa masuala ya mitindo na wanamitindo wa
ndani, Evelyn Rugemarila si jina geni masikioni mwao. Kupitia lebo yake ya Eve Collections,
Evelyn ameingia kwenye orodha ya wabunifu wa mavazi ya wanawake wanaofanya
vizuri kwa sasa nchini Tanzania.
“Siku zote nimekuwa naamini
nachokifanya na kukubali
kujifunza kutoka kwa watu wengine,” anasema Evelyn katika mahojiano na Johari.
“Kuna wakati unaweza kutamani kufanya kitu, lakini wewe
mwenyewe ukajikatisha tamaa. Wengi wanakosea hapo hasa wanawake.
“Binafsi nilijiamini wakati naanza kazi hii ndiyo maana
nimeweza kusimama mpaka leo na najivunia kuwa miongoni mwa wabunifu mahiri
nchini Tanzania,” anasema mbunifu huyo.
Safari yake kuelekea kuwa mbunifu
“Nilimuelezea wazo langu mama yangu namshukuru Mungu
alinielewa na kuniunga mkono kwa kunipatia fedha. Nikaagiza vifaa China na
kuanza kufuata malighafi za vitambaa Nigeria.”
Mtazamo wake katika tasnia ya mitindo
Evelyn anaelezea kuwa kuna maendeleo makubwa katika
tasnia hii ambayo kwa sasa inaonekana kuanza kuingia vichwani mwa Watanzania
wengi.
Anaeleza kuwa kumekuwepo na ongezeko la wabunifu ambao
wanajitahidi kutengeneza nguo mbalimbali na Watanzania kwa kiasi fulani
wameanza kuonyesha muamko wa kupenda kazi za nyumbani.
Pamoja na mafanikio hayo, Evelyn anasema kuwa bado kuna
watu wanaojiita wabunifu lakini hakuna
ubunifu wanaofanya na matokeo yake wanaiga mitindo ya wengine.
“Nasema hivyo kwa ushahidi. Kuna watu nawafahamu fika
kuwa wanakubali kuchukua mitindo yangu kutoka kwa wateja na kuwashonea kwa
gharama nafuu.
Kutokana na ukweli huo ni ngumu kwa tasnia yetu kukua na
kuyafikia mataifa mengine kama wenzetu Nigeria. Kule kila mbunifu ana ladha
yake na hakuna anayekubali kuiga kazi ya mwenzake,” anasisitiza.
Anafafanua kuwa kwa uzoefu wake wa kutembelea nchi
mbalimbali amegundua kuwa watu wengi wanaojihusisha na ubunifu wamesomea na
kuwekeza fedha za kutosha kwenye kazi zao.
“Mataifa mengine huwezi kuwa mbunifu bila kuwa na elimu
au kuwekeza fedha za kutosha kutafuta malighafi nzuri na sio kubabaisha kama
ambavyo wengi wanafanya hapa nchini,” anafafanua.
Mwanamama huyo anasema mpaka sasa ameshashiriki maonyesho mawili ya mitindo nje
ya nchi na kufanikiwa kuzitangaza nguo zake ambazo kwa kiasi kikubwa hutawaliwa
na nakshi za Kiafrika.
Historia kwa ufupi
Evelyn alizaliwa Desemba 1971, mjini Muleba akiwa ni
mtoto wa kwanza katika familia ya watoto watatu ya mfanyabiashara maarufu
nchini, James Rugemarila.
Evelyn anasema alijikuta katika tasnia hiyo baada ya
kushindwa kupata nguo zinazoendana na mwili wake.
Evelyn anaeleza kuwa unene wa mwili wake ulimuweka katika
wakati mgumu kupata nguo zinazomtosha na kumkaa vizuri mwilini.
“Napenda kuvaa vizuri lakini nilikuwa sipati nguo
zinazonikaa kwa jinsi ninavyopenda mpaka nilivyokwenda kumtembelea ndugu yangu
nchini Nigeria,” anasema.
Anasema akiwa Nigeria alivutiwa na namna wabunifu wa nchi
hiyo walivyokuwa wakitengeneza nguo zao kwa kutumia vitambaa vyenye nakshi za
kuvutia.
“Binafsi nilipenda jinsi walivyonishonea nguo ambazo
zilinikaa vizuri kwenye mwili ambao mpaka wakati huo ilikuwa ngumu kupata vazi
linalonipendeza kutokana na unene”.
Aliporejea nyumbani watu wengi walionyesha kuzipenda nguo
hizo na kumshawishi kubuni mavazi kwa kutumia malighafi za vitambaa kutoka
Nigeria.
Kwa kuwa alikuwa na mapenzi na ushonaji, akaona ni vyema
akaifanya kazi hiyo kwa kiwango cha ubora zaidi kwa kuwalenga watu wenye
maumbile makubwa.
Elimu ya msingi aliipata Shule ya Msingi ya Mlimani
jijini Dar es Salaam na kisha kuhamia Arusha alikomalizia darasa la saba.
Baada ya kuhitimu elimu ya msingi alijiunga na masomo ya
kidato cha kwanza nchini Kenya ambako alisoma mpaka kidato cha tano.
Alikwenda Uingereza katika Chuo cha Reden alikojiunga na
kidato cha sita kisha kuunganisha elimu ya shahada ya sosholojia chuoni hapo.
Huo haukuwa mwisho wa safari ya elimu, kwani aliendelea
na stashahada ya utawala katika Chuo Kikuu cha East London kisha kendelea na
Shahada ya juu Chuo Kikuu cha West Minister.
Baada ya kumaliza masomo yake Evelyn alirejea nyumbani na kujihusisha na biashara
za familia yake ambayo kwa wakati huo walikuwa na kampuni iliyokuwa ikijihusisha na uingizaji na usambazaji wa bia ya Heineken
nchini.
MWANANCHI
No comments:
Post a Comment