Wananchi wakivushana eneo la jangwani |
HALI tete imelikumba jiji la Dar es Salaam kufuatia mvua
kubwa inayoendelea kunyesha tokea jana kiasi cha kusababisha mafuriko hasa
katika maeneo ya mabonde huku familia nyingi zikikosa makazi baada ya nyumba
wanazoishi kujaa maji.
Kufuatia hali hii Serikali imetangaza kuifunga kwa muda
barabara ya
Jangwani baada ya eneo hilo kujaa maji kiasi kwamba hakuna gari
inayoweza kuingia wala kutoka.
Eneo la jangwani na Posta yametajwa kuwa Miongoni mwa
maeneo ambayo yameathirika zaidi na mvua hii, na maeneo mengine ni Bonde la
Mpunga Msasani, Mwananyamala, na Masaki.
Inadaiwa kuwa nyumba nyingi zimejaa maji kiasi cha
kuwafanya watu kuhama makazi yao huku wakipoteza thamani zao zilizokuwa ndani
ya nyumba zao.
Maeneo mengine ni yale ambayo mto Msimbazi umepita,
ambapo wakazi wengi wanaokaa kandokando ya mto huo wameathiriwa vibaya na mvua
baada ya mto huo kujaa na kuanza kuingia kwenye makazi ya watu.
Pamoja na kunyesha kwa mvua hiyo, hadi majira haya hakuna
taarifa za kifo zilizotolewa, aidha vyombo vya usalama vimeendelea kutoa msaada
kwa waathiriaka mbalimbali wa mafuriko hayo.
wakazi wa eneo la Sinza hasa katika eneo la Bamaga,
wamesikitishwa na kitendo cha watu kuziba mitaro kwa kutupa takataka ovyo,
wakieleza kuwa hicho ndiyo chanzo cha kufurika kwa maji katika mitaa yao jambo
ambalo limesababisha adha kubwa.
Eneo lingine ambalo limeathirika ni Kinondoni ambapo
wananchi wa maeneo ya mabonde wanalalamika kuchelewa kutoa vitu vyao ndani,
kwani asilimia kubwa ya wakazi hao mali zao zimezama ndani ya vyumba vyao.
Maeneo mengine ambayo wananchi wa jiji la Dar es Salaam
wanaendelea kuhaha ni pamoja na eneo la
Mabibo, Tandale, Tabata, Mwananyamala Kisiwani, kwa Kopa, Tabata
Kinyerezi, na eneo la posta ambapo ofisi nyingi zimeonekana kuzingirwa na maji
huku hali ya sintofahamu ikitawa.
Pamoja na kuendelea kunyesha kwa mvua hiyo vijana wa kazi
wamekuwa wakijipatia ridhiki kwa kuwavusha watu maeneo mbalimbali kwa gharama
ya kati ya Sh500 hadi 1000, tuvuti hii ilipozungumza nao walijieleza kuwa wapo
tayari kuwasaidia watu, kuwavusha maeneo mbalimbali na pindi wanapofanya hivyo
hupewa fedha za shukrani.
“Hatuwezi kuomba mvua iendelee kunyesha, kwani inaleta
usumbufu mkubwa wa watu, pia mali nyingi kupotea, hii ni kazi ya Mungu, na sisi
tunapata riziki humuhumu, tunasaidia kuwavusha watu, pia kusukuma magari
yanapokwama, tunapofanya hivi tunapewa pesa kidogo kati ya Sh 500 hadi
1000”, amesema kijana mmoja katika eneo
la Jangwani.
Aidha wataalamu wa hali ya hewa wanaeleza wazi kuwa kama
mvua ikiendelea kunyesha kwa muda wa siku tatu ama nne mfululizo madhara
amakubwa yanaweza kujitokeza katika jiji la Dar es Salaam kufuatia kuziba kwa
miundombinu ya kupitisha maji.
Aidha sababu nyingine iliyotajwa ni wananchi kuvamia na
kujenga kandokando ya mito na mabwawa ambayo awali yalikuwa yanasaidia
kuhifadhi maji ili yasiwadhuru wananchi..
MWANANCHI
No comments:
Post a Comment