MEYA wa Manispaa ya Kinondoni, Yusuph Mwenda amekabidhiwa
tuzo ya kuwa meya bora barani Afrika.
Tuzo hiyo alikabidhiwa jijini Dar es Salaam jana na
Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu na Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa
(Tamisemi), Hawa Ghasia.
Meya Mwenda amefanikiwa kupata tuzo hiyo katika kundi la
mamlaka za miji ya kati ambayo ina majiji yenye idadi ya watu isiyozidi milioni
moja.
Akitaja sifa za tuzo hiyo, Mkurugenzi wa Manispaa ya
Kinondoni, Mhandisi Mussa Natty, alisema vigezo hivyo ni pamoja na uongozi na
dira katika utoaji wa huduma kuchochea maendeleo, uadilifu, ubunifu na
usimamizi bora wa shughuli za halmashauri.
Natty alisema sifa nyingine ni uhamasishaji wa jamii
katika kushiriki masuala ya halmashauri, uwezo wa kuchochea maendeleo ya
kiuchumi na kijamii, uwezo wa kusimamia ulinzi na usalama wa wananchi ikiwamo
kujenga mahusiano mazuri katika jamii.
Mamlaka ya miji iliyoshinda na tuzo kwenye mabano ni
Accra, Ghana (majiji makubwa), Kinondoni, Tanzania (majiji ya kati) na Praia,
Cape Verde (majiji madogo).
Zawadi alizokabidhiwa Mwenda ni kikombe, cheti na fedha
taslim kiasi cha dola za Marekani 100,000 sawa na Sh milioni 200.
Waziri Ghasia aliipongeza halmashauri hiyo ikiwamo na
kuishauri kutumia zawadi ya fedha walizopata kuzalisha ajira kwa vijana na
akina mama wa Kinondoni.
MTANZANIA
No comments:
Post a Comment