Raia watatu wa Ugiriki na Mtanzania mmoja wamepandishwa
kizimbani katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu wakikabiliwa na shtaka la
kughushi muhuri wa Mkuu wa Jeshi Polisi
Nchini (IGP).
Washtakiwa hao ni
Lalvin Kawa mfanyakazi wa Kampuni ya Simu ya Airtel,
na raia wa Ugiriki;
Athasios Vogiatzis (31), Panagiotis Angelidis (29) na Fotios Vogiatzsis (29).
Akisoma hati ya mashtaka
jana, Wakili wa Serikali, Mununila Munisi alidai mbele ya Hakimu Mkazi, Emilius Mchaulu kuwa washtakiwa walitenda kosa hilo katika
tarehe na muda usiofahamika wilayani Ilala.
Alidai kwamba katika shtaka la kwanza washtakiwa hao kwa
pamoja kwa nia ovu, walighushi muhuri huo wa IGP wakionyesha ni halali na
umetolewa na Jeshi la Polisi la Tanzania wakati wakijua si kweli.
Shtaka la pili wanadaiwa kuwa katika tarehe
zisizofahamika jijini Dar es Salaam, walighushi taarifa ya upotevu wa mali
inayotolewa na jeshi hilo la polisi
wakionyesha ni halali na imetolewa na
polisi wakati wakijua siyo kweli.
Washtakiwa wote walikana mashtaka hayo na upande wa
mashtaka ulidai upelelezi wa kesi hiyo haujakamilika na kuomba ipangwe tarehe
nyingine.
Hakimu aliwataka washtakiwa hao wawe na wadhamini wawili
wa kuaminika na kila mmoja atasaini bondi ya Sh5 milioni .
Pia, washtakiwa hao hawaruhusiwi kutoka nje ya Mkoa wa
Dar es Salaam bila kibali cha mahakama na wametakiwa kuwasilisha hati zao za kusafiria.
Washtakiwa wote walishindwa kutimiza masharti hayo na
hivyo wamerudishwa rumande. Kesi imeahirishwa hadi Mei 18, 2015.
MWANANCHI
No comments:
Post a Comment