Mbunge wa Bariadi Magharibi, Andrew Chenge, amefungua
kesi ya kikatiba dhidi ya Baraza la Maadili ya Viongozi wa Umma na maazimio ya
Bunge kuhusiana na malalamiko ya ukiukaji wa maadili ya uongozi.
Chenge, anatuhumiwa kupokea
fedha kutoka kwa Kampuni ya
VIP Engineering and Marketing Ltd Sh. bilioni 1.6.
Chenge aliitwa katika Baraza la Maadili ya Viongozi wa
Umma kuhojiwa kuhusiana na tuhuma hizo ambazo ni kinyume cha maadili. Hata
hivyo, alipinga akisema kuwa baraza hilo halina mamlaka ya kumhoji kwa kuwa
liko katika Mahakama ambayo ina mamlaka kuliko baraza, na kueleza kuwa
atafungua kesi ya kupinga mahakamani.
Katika maombi yake, lililowasilishwa masjala kuu ya
Mahakama Kuu Tanzania, Kanda ya Dar es Salaam, Chenge ameorodhesha sababu 13 za
kupinga mwenendo wa baraza na
mapendekezo yaliyowasilishwa na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) na
Kamati ya Bunge na Hesabu za Serikali (PAC) kuhusiana na shauri hilo.
Kwa mujibu wa hati yake ya maombi, anadai kwamba mwenendo
wa Baraza na maazimio ya Bunge ya Novemba 29, mwaka 2014, yalikuwa ni kinyume
cha amri iliyotolewa Novemba 25, mwaka 2014 ikisimamisha kwa muda kuwasilishwa
na majadiliano ripoti iliyohusiana na uhamishaji wa fedha za akaunti ya Tegeta
Escrow.
Kesi hiyo imepangwa mbele ya jopo la majaji watatu
likiongozwa na Stella Mugasha, Augustine Mwarija na Dk. Fauz Twaib.
Majaji wamewaelekeza walalamikiwa ambao ni Tume ya
Maadili ya Baraza la Maadili na
Mwanasheria Mkuu wa Serikali kuwasilisha majibu yao Mei 8 na Mei 21, mwaka huu
kesi hiyo itasikilizwa.
Jopo la mawakili 10 linalomwakilisha Chenge katika kesi
hiyo linawajumuisha Deogratias Ringia, Wilson Ogunde, Jamhuri Johnson, Michael
Ngalo, Respicius Didace, Okare Emesu, Cuthbert Tenga, Dosca Mutabuzi, John
Nyange na Stephano Kamala.
Katika maombi yake, Chenge anaiomba mahakama kutoa amri
ya kudumu ya kuizuia Tume na Baraza kuendelea au kutafakari kuanzisha malalamiko yoyote dhidi
yake kuhusiana na ripoti za CAG na PAC.
Kadhalika, anaiomba mahakama kutoa azimio kwamba malalamiko yaliyoanzishwa na tume
kupitia baraza lake ni batili kutokana
na ukiukaji wa taratibu na kwamba majadiliano ya Bunge na maazimio yake
hayakuwa sahihi, hayakuwa ya kisheria, na kwa hiyo yalikuwa batili.
NIPASHE
No comments:
Post a Comment