Matanuzi ni sehemu ya maisha ya mastaa wengi duniani,
hivyo hata wanapoamua kufanya mambo ya maendeleo, hukakikisha wanafanya yale
yatakayoendana na hadhi zao. Wapo wanaoamua kutanua kwa akili kwa kuwekeza
katika vitu vya msingi kama nyumba na vitega uchumi.
Tofauti na miaka iliyopita, mastaa wa Bongo, sasa
hujiona
wamefanikiwa ikiwa watamiliki ardhi au nyumba za kifahari tofauti na miaka ya
nyuma.
Leo hii hata wanaomiliki magari makali, ukiwachunguza kwa
undani utagundua tayari wameshawekeza katika ardhi na wameshaanza ujenzi wa
nyumba za kifahari.
Starehe inakuletea orodha mastaa 10 wa Bongo wanaomiliki
nyumba za kisasa, zenye thamani kubwa. Orodha hii haina haijazingatia nafasi
zao.
Lady Jaydee
Ni msanii anayejiheshimu na aliyejijengea imani kubwa kwa
mashabiki wake na wapenzi wa muziki Afrika. Fedha yake ya awali kabisa
aliyoichuma kupitia muziki, aliwekeza kwenye ardhi na kuwa msanii wa kwanza
Bongo aliyemiliki nyumba ghali maeneo ya Kimara jijini Dar es Salaam. Hata
hivyo, hakuwahi kutangaza thamani ya nyumba hiyo. Pia anatajwa kumiliki mali
kadhaa.
Profesa Jay
Aliwahi kutangaza kwamba nyumba yake aliyoijenga Mbezi ya
Kimara jijini Dar es Salaam ina thamani ya Sh100 milioni. Huyu alikuwa miongoni
mwa wasanii wa mwanzo kabisa kutangaza kumiliki nyumba zao wenyewe, hali
iliyoongeza mwamko kwa wasanii wengine wachanga kuwekeza katika ardhi.
Madee
Ni mwanamuziki mkongwe kutokea katika kundi la Tiptop
Connection. Pia anajulikana zaidi kwa jina la Rais wa Manzese, anamiliki nyumba
ya kisasa iliyopo maeneo ya Mbezi, Dar es Salaam. Ni nyumba ambayo hajawahi
kutaja kiasi cha fedha halisi kilichotumika kuikamilisha licha ya kuonekana
kuwa imegharimu fedha nyingi.
Diamond
Mwaka 2015 umekuwa ni mwaka wa staa huyu baada ya
kufanikiwa kuhamia katika nyumba yake iliyopo katika eneo la wa Madale Tegeta,
Dar es Salaam. Nyumba hiyo ambayo imedaiwa kuwa na choo kilichonakshiwa kwa
dhahabu yenye thamani ya Sh 70 milioni
Kwa mujibu wa msanii huyo, nyumba hiyo imegharimu zaidi
ya Sh280 milioni, imechukua takribani miaka miwili kumalizika na ina bwawa la
kuogelea, Gym, Dancing Hall, Studio, DartsCourt na BasketBall Court.
Nay wa Mitego
Ni mwanamuziki wa hiphop ambaye amefanikiwa kuwajuza
mashabiki kwamba aina hiyo ya muziki kwa sasa inalipa baada ya kujenga nyumba
ya kifahari iliyogharimu kiasi cha Sh180 milioni. Kwa mujibu wa Ney wa Mitego,
alianza kujenga nyumba hii tangu mwaka 2013 na ni miongoni mwa nyumba zake
tatu, huku nyumba zake mbili zikiwa bado hazijakamilika.
Masanja Mkandamizaji
Licha ya kumiliki mashamba makubwa ya mpunga na miradi
kadhaa, Masanja Mkandamizaji anamiliki nyumba tatu za maana Dar es Salaam, moja
ni ghorofa iliyopo maeneo ya Tabata, nyingine Kigamboni na nyingine haifahamiki
eneo ilipo.
Hata hivyo, imebainika kuwa mbali na mijengo yake hiyo ,
nyumbani kwao Mbarali, Mbeya ana mjengo wa maana.
Juma Jux
Mwanamuziki Juma Jux yeye ni mmoja kati ya wasanii
waliofanikiwa kupitia kazi zao za sanaa, baada ya kujenga jumba la kifahari
lenye ghorofa moja ambalo mpaka sasa bado haijajulikana liko eneo gani jijini
Dar es Salaam. Kwa mujibu wa Jux, jumba hilo litakuwa na studio, bwawa la
kuogelea, gym na sehemu zingine muziki kama alivyotangaza.
Chege na Temba
Hawa ni wasanii wanaotokea katika kundi la TMK Wanaume
Family lililo chini ya Said Fella. Wawili hawa wanamiliki nyumba mbili kila
mmoja. Fella anasema amekuwa akifanya hivyo kwa wasanii wengine ambao
walishatoka ndani ya kundi hilo wapatao saba.
“Nilishawakabidhi waliotoka sitaki kuwataja kila siku
maana wananambiaga kwanini nawataja, lakini nishafanya hivi kwa wasanii wangu
siyo chini ya saba. Thamani yake bado hatujakaa kupiga mahesabu maana ujenzi
wake ni wa kimaskini na ufahamu tukipata Sh102,000; Sh20,000 tunanunua matofali
na Sh80,000 tunakula na watoto. Ina vyumba vitatu vya kulala, sehemu ya
chakula, parking ya magari. Temba na Chegge wana nyumba mbili mbili,” anasema
Fella
Idris Sultan
Mshindi wa Big Brother Hotshots aliyefanikiwa kujipatia
kitita cha dola za Marekani 300,000 hivi sasa anamiliki jumba lenya ghorofa
moja. Hata hivyo, nyumba hiyo bado hajazungumzia kuhusu gharama halisi
alizotumia kuinunua.
AY
Huyu ni kati ya wasanii wanaomiliki fedha, kampuni na
mali kibao lakini hawapendi kujionyesha imefahamika. Chanzo makini na cha
karibu na msanii huyo kimesema kuwa AY ni msanii anayemiliki biashara nyingi
ndani na nje ya nchi.
Anadaiwa kumiliki nyumba na viwanja kadhaa hapa jijini
sambamba na maduka kadhaa Nairobi Kenya.
AY aliwahi kukaririwa akisema kuwa ana mpango wa kununua
nyumba Kenya na kufungua maduka kwakuwa ni sehemu ambayo anakwenda sana kwa
ajili ya shughuli zake mbalimbali.
MWANANCHI
No comments:
Post a Comment