Kiganja cha mtoto Baraka Cosmas (6) mwenye ulemavu wa
ngozi (albino) kilichokatwa Machi 8 kwenye Kijiji cha Kipeta, Sumbawanga
Vijijini kimepatikana mwishoni mwa wiki wilayani Mbozi.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mbeya,
Ahmed Msangi alisema
juzi mjini hapa kwamba kiganja hicho kilipatikana kutoka kwa mkazi wa Kijiji
cha Malonje, Sajenti Kalinga (54) ambaye anafanya kazi ya useremala.
Alisema awali, polisi walimkamata mganga wa kupiga ramli
aliyemtaja kwa jina la Gunela Shinji wa Kijiji cha Kipeta kuwa ndiye
aliyehusika kukata kiganja hicho.
Alisema baada ya kumbana mganga huyo alimtaja Kalinga
kwamba ndiye aliyemtuma kuleta kiganja hicho cha mtu mwenye ulemavu wa ngozi
(albino).
“Tulimbana mtuhumiwa akatueleza kuwa aliyemtuma kiganja
hicho ni Sajenti Kalinga kwa dau la Sh100 milioni,” alisema Msangi.
Kamanda Msangi alisema mtuhumiwa Shinji aliwapeleka
polisi hadi kwa mteja wake huyo na kufanikiwa kumkamata.
“Polisi walifika nyumbani kwa mtuhumiwa Kalinga na
walipomhoji kwa kina, alikitoa kiganja hicho na kuwakabidhi.”
Alisema hadi juzi, watu sita walikuwa wanashikiliwa kwa
tuhuma za kuhusika na tukio hilo wakiwamo waliokamatwa mwaka jana na wengine
mwaka huu.
Wanaoshikiliwa ni baba wa mtoto huyo, Cosmas Lusambo,
mganga wa jadi, Miambo Kameta; Shinji na Kalinga.
Mtoto Baraka Cosmas aliyekatwa kiganja hicho amelazwa
katika Hospitali ya Rufaa Mbeya akiendelea na matibabu chini ya uangalizi wa
mama yake Prisca Shaaban (28) ambaye sasa ana watoto watano, wanne kati yao
wakiwa albino.
Mama huyo alisema amepata taarifa za kukamatwa kwa
watuhumiwa hao na kwamba ingawa hajui masuala ya kisheria, anaamini Serikali
itachukua hatua stahiki kwa watakaobainika kuhusika.
Msangi alisema watuhumiwa hao watafikishwa mahakamani
mkoani Rukwa wakati wowote.
MWANANCHI
No comments:
Post a Comment