WATU wanaosadikiwa kuwa ni majambazi wamebomoa kaburi la
Napegwa Kishaluli (75) mkazi wa Mailimoja Kibaha mkoani Pwani aliyezikwa Aprili
20 mwaka huu na kumvua nguo zote pamoja na kuchukua mikoba aliyokuwa amezikwa
nayo.
Mkataba wa mlinzi huyo ulipomalizika aliondoka na siku
iliyofuata kaburi hilo lilivunjwa.
Watu wa karibu na familia ya marehemu waliliambia MTANZANIA
kuwa baada ya mazishi ulikuwapo uvumi kwamba marehemu alizikwa na vitu vya
thamani zikiwamo fedha, simu, pete na mikufu ya dhahabu pamoja na nguo zenye
thamani kubwa.
Hata hivyo, taarifa zinasema marehemu Kishaluli alizikwa na
mikoba miwili ya nguo na vitu vyake vingine na kwamba kabla ya kifo chake
aliagiza azikwe na vitu vyake.
Akizungumza na MTANZANIA jana,ndugu wa marehemu,Bartholomew
Mwanjile alisema baada kuzika walilazimika kuajiri mtu wa kulinda kaburi hilo
la ndugu yao kwa wiki moja lakini siku moja baada ya mkataba kumalizika kaburi
hilo lilivunjwa.
“Tuliweka mlinzi alinde kaburi hilo kwa wiki moja tukiamini
litakuwa limekauka kwa sababu lilitengenezwa kwa zege.
“Tuliamini watu wenye nia mbaya watashindwa kulivunja jambo
ambalo limekuwa kinyume kwa vile baada ya muda huo kumalizika kaburi
lilibomolewa na watu wasiojulikana ambao waliamini ndani ya mikoba hiyo
kulikuwa na fedha,” alisema Mwanjile.
Mwanjile alisema baada ya kuvunja kaburi hilo majambazi
walifungua jeneza na kupekua ndani kwa kuligeuza na kuliweka tofauti na
lilivyokuwa awali, baada ya kumvua marehemu nguo zote na viatu alivyokua
amevalishwa na hata soksi nazo walichukua.
Alisema tukio la kuvunjwa kwa kaburi hilo limetokea baada ya
uvumi kuwa ndugu yao alizikwa na nguo na vitu vingine zikiwamo fedha, kiasi cha
Sh milioni 8, cheni ya dhahabu,simu za gharama na kompyuta
mpakato(laptop),jambo ambalo si la kweli.
“Tulimzika ndugu yetu na mikoba ya nguo zake ambazo aliagiza
kabla ya mauti kumkuta na kaburi tulijenga kwa zege lakini tukashauriana tuweke
mlinzi, hapo ndipo watu wakaanza kutia shaka wakadhani kuna vitu vya gharama
jambo ambalo si kweli,” alisema Mwanjile.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Pwani, Jafari Mohamedi
alithibitisha kutokea kwa tukio hilo na kwamba uchunguzi unaendelea na
watakaobainika watachukuliwa hatua za sheria.
No comments:
Post a Comment