SERIKALI imesema Watanzania 23 wamenusurika kuuawa katika
ghasia zinazoendelea nchini Afrika Kusini baada ya kujificha kwenye duka kubwa
(Supermarket).
Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam
jana, Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Bernard Membe,
alisema hadi jana hakuna taarifa za Mtanzania aliyepoteza maisha.
Alisema katika vurugu hizo, watu wanane ambao walifariki
dunia wanatoka nchi za Malawi, Msumbiji, Ethiopia, Zimbambe, Swaziland na
Somalia.
Alisema baada ya Serikali kupata taarifa hizo,
waliwasiliana na Serikali ya Afrika Kusini pamoja na ubalozi wa Tanzania nchini
humo ili kupata taarifa kamili kuhusu suala hilo.
“Tuliwasiliana na ubalozi wetu kwa kushirikiana na
Serikali ya Afrika Kusini, wametuhakikishia hakuna Mtanzania hata mmoja
aliyefariki dunia katika vurugu hizo,” alisema Membe.
Hata hivyo, alisema kuna taarifa ya vifo vya Watanzania
watatu waliofariki dunia katika matukio tofauti na majina yao yamekuwa
yakisambazwa kwenye mitandao ya kijamii.
Aliwataja kuwa ni Ali Hashim Mohamed aliyefariki kwa
ugonjwa wa kifua kikuu (TB) ambaye mwili wake umewasili nchini juzi na Athuman
China Mapepo aliyefariki baada ya kuchomwa visu kwenye vurugu zilizotokea ndani
ya gereza, akitumikia kifungo baada ya kushtakiwa kwa kosa la jinai.
Mwingine ni Rashid Jumanne ambaye aliuawa baada ya
kushiriki tukio la wizi kwenye nyumba ya mtu.
Alisema baada ya kutokea vurugu hizo, zaidi ya wananchi
3,000 kutoka mataifa mbalimbali walikimbilia kwenye kambi ya ‘Supermarket’ ili
kunusuru maisha yao.
“Tayari tumewatuma maofisa ubalozi nchini Afrika Kusini
kuzungumza na Watanzania waliopo kwenye kambi hiyo ili waweze kupata taarifa
kamili juu ya mgogoro huo.
“Baada ya mazungumzo hayo, kati yao 21 wamekubali kurudi
nyumbani, lakini wawili wamekataa,” alisema.
Alisema Tanzania inaunga mkono kauli ya Mwenyekiti wa
Umoja wa Afrika (AU) ambaye pia ni Rais wa Zimbabwe, Robert Mugabe kulaani na
kupinga vurugu hizo na kuitaka Serikali ya Afrika Kusini kuongeza juhudi za
kuchukua hatua.
MTANZANIA
No comments:
Post a Comment