Saturday, April 18, 2015

Vurugu Afrika Kusini zadaiwa kuua Mtanzania....Ubalozi wakana

Baadhi ya Watanzania wanaoishi Afrika Kusini wamedai kuwa mwenzao mmoja amefariki dunia kutokana na vurugu zinazoendelea nchini humo.

Hata hivyo, Kaimu Balozi wa Tanzania nchini Afrika Kusini, Elibahati Lowassa
alisema hadi kufikia jana hawakuwa na taarifa ya Mtanzania yeyote kujeruhiwa wala kupoteza maisha katika vurugu hizo.

Balozi Lowassa alisema ubalozi upo tayari kuwarejesha nyumbani raia wake waliokwama kutokana na machafuko hayo.

Wakati ubalozi ukisema hayo, Watanzania wanaoishi nchini humo walizungumza na gazeti hili kwa njia ya simu kuhusiana na madai hayo.

Mkazi wa Cape Town, Afrika Kusini, Mohamed Khatib alisema Mtanzania huyo alipigwa hadi kufa wakati vurugu hizo zilipokuwa zinaendelea juzi jioni.

“Hizo ni taarifa za kuthibitika. Huyo mwenzetu alikuwa anaishi Durban ambako vurugu zilikithiri sana,” alisema Khatib na kuongeza:

“Hata hivyo, kuna uwezekano wapo majeruhi kwa sababu hali ni mbaya na tunashangaa ubalozi wetu hausemi chochote kuhusu hili...upo kimya tu.”

Mkazi wa Durban, Denis Gabriel alisema tangu juzi usiku, katika eneo hilo kulitawaliwa na raia wa nchi hiyo kuwashambulia wageni.

“Ilikuwa wakikutana na mtu ambaye si raia mwenzao, wanampiga, wanavamia na kuvunja maduka, wanavunja vioo vya magari ya wageni, lakini tunashukuru Mungu baadaye polisi walifika na kutuliza ghasia,” alisema Gabriel anayefanya biashara ya kuuza bidhaa kwenye duka la vifaa vya umeme.

“ Hali ni shwari kiasi japokuwa hadi sasa hatujapata taarifa kama kuna Mtanzania aliyefarikia au kujeruhiwa kutokana na vurugu hizo, lakini inawezekana wapo . Hatuna taarira kwa sababu watu hatutoki ndani kila mtu anahofia usalama wake.

“Hatuna amani kwa sababu ya hizo virugu, jana (juzi) wanaofanya vurugu walikuwa Durban, tumesikia leo wanakuja Johanesburg,” alisema dada aliyejitambulisha kwa jina moja la Lorah ambaye anafanya kazi nchini humo.

Jana, vyombo mbalimbali vya habari vya nchini humo likiwemo gazeti la Mail and Guardian viliripoti polisi wameimarisha ulinzi hasa katika mji wa Johannesbarg.
Mkazi mwingine, George Okello alisema zaidi ya raia wa kigeni 2000 wanaishi kwenye makambi kwa kuhofia usalama wao.

“Serikali yao imeamua kuwapeleka huko wakiwa na ulinzi hadi kuwe na utulivu, hawa jamaa hawafai wanachoma hadi nyumba,” alisema.

Alisema kutokana na hali hiyo, baadhi ya raia wa kigeni wanalazimika kujifungia ndani.

Hata hivyo, Ofisa habari wa Wazara ya Mambo ya Nje, Ally Mkumbwa alisema hakuna hatua yoyote iliyochukuliwa hadi sasa kutokana na kutokuwapo kwa taarifa rasmi kutoka ubalozini.

“Hatujapata taarifa rasmi kutoka kwa viongozi wa ubalozi wetu. Tunasubiri, wakituma taarifa ndipo tutajua tuchukue hatua gani, lakini kwa sasa hatuwezi kufanya chochote,” alisema Mkumbwa.

MWANANCHI

No comments:

Post a Comment