MSAIDIZI wa Kiongozi wa Kanisa la Ufufuo na Uzima,
Josephat Gwajima, George Mzava, amepandishwa kizimbani katika Mahakama ya
Hakimu Mkazi Kisutu.
Mzava (43), mfanyabiashara na mkazi wa Ilala, Dar es
Salaam, alifikishwa mahakamani hapo jana
na kusomewa mashitaka ya kukutwa na bastola ya kiongozi huyo na risasi kinyume
cha sheria.
Wakili wa Serikali Mwandamizi, Tumaini Kweka, alimsomea
Mzava mashitaka hayo mbele ya Hakimu Mkazi, Wilfred Dyansobera, baada ya
mshitakiwa huyo kujisalimisha.
Mzava akisindikizwa na wakili wake, Peter Kibatala,
alifika mahakamani hapo ili kusomewa mashitaka yanayomkabili katika kesi
iliyofunguliwa Ijumaa iliyopita, ambayo washitakiwa wenzake watatu, akiwemo
Gwajima, walisomewa mashitaka yao.
Washitakiwa wengine katika kesi hiyo, ambao walisomewa
mashitaka yanayowakabili Ijumaa na kuachiwa kwa dhamana ni Askofu Msaidizi
Yekonia Bihagaze na Mchungaji Geoffrey Milulu.
Katika kesi hiyo, washitakiwa wote wanne wanakabiliwa na
mashitaka matatu. Gwajima anakabiliwa na
shitaka la kushindwa kuhifadhi silaha na risasi anazomiliki kihalali katika
usalama huku wengine wakidaiwa kukutwa nazo kinyume cha sheria.
Akimsomea mashitaka yanayomkabili Mzava, Kweka alidai
Machi 29, mwaka huu, katika Hospitali ya TMJ, Mikocheni A, jijini Dar es
Salaam, mshitakiwa huyo na wenzake, Bihagaze na Milulu, walikutwa na bastola
aina ya Bereta bila kuwa na kibali au
ruhusa kutoka katika mamlaka zinazohusika.
Katika shitaka la pili, Mzava na wenzake hao wanadaiwa
siku hiyo wakiwa hospitalini hapo, walikutwa na risasi tatu za bastola na 17 za
bunduki aina ya shotgun bila kuwa na kibali au ruhusa kutoka mamlaka
zinazohusika.
Mshitakiwa huyo alikana mashitaka hayo, ambapo Wakili
Kweka alidai upelelezi haujakamilika na kuomba shauri hilo kuahirishwa hadi
tarehe nyingine kwa kutajwa.
Hakimu Dyansobera alitoa masharti ya dhamana kwa kumtaka
mshitakiwa kutia saini dhamana ya sh. milioni moja na kuwa na mdhamini mmoja
mwaminifu atakayetia saini dhamana ya kiasi hicho.
Mshitakiwa alitimiza masharti hayo, hivyo aliachiwa kwa
dhamana hadi Mei 4, mwaka huu, kesi itakapotajwa.
UHURU ONLINE
No comments:
Post a Comment