DUKA la jumla (Supermarket) lijulikanalo kwa jina la
Huarang lililopo Dar es Salaam linalomilikiwa na raia wa China, limejiwekea
mazingira ya kupiga vita Watanzania wenye ngozi nyeusi kuingia ndani na kununua
bidhaa.
Duka hilo liko katika Mtaa wa Ursino, Mikocheni katika
kitalu namba 56 na mwandishi wa habari hizi ni miongoni mwa waathirika wa
ubaguzi ambao ni wa aina yake hapa nchini.
Gazeti hili lilikuwa limepata taarifa kutoka katika
vyanzo vyake vya habari kuhusu duka hilo na juzi Jumatatu waandishi wa gazeti
hili walikwenda wenyewe kujionea nini hasa kinafanyika katika eneo hilo.
Kwa nje, duka hilo halina dalili kwamba linafanya
shughuli hizo kwani limezungukwa na nyumba inayoonekana kama makazi ya kawaida
ya watu kuishi, lakini mtu anapoingia ndani ndiyo ataona duka hilo ambalo huuza
vyakula na vinywaji baridi vinavyopenda kutumiwa na watu wenye asili ya China.
Hapo awali, mmoja wa watu waliowahi kukumbwa na kadhia
hiyo ya ubaguzi alilieleza gazeti hili namna alivyozuiliwa kuingia ndani ya
duka hilo kwa maelezo kwamba hairuhusiwi.
“Ili gari yako iruhusiwe kuingia ndani ya duka hilo ni
lazima uwe umempakiza mtu mwenye asili ya China la sivyo hawaruhusu. Mimi
niliambiwa tu na nilipokwenda kujaribu nilikataliwa kuingia kwa madai kuwa
siruhusiwi,” alisema mmoja wa waathirika wa ubaguzi huo ambao hata hivyo
hakutaka kutajwa jina lake.
Waandishi wawili wa Raia Mwema waliingia katika eneo hilo
kwa kutumia gari la ofisi lenye nembo ya kampuni lakini walipofika getini
waliombwa na mlinzi wa kampuni ya ulinzi ya KK Security kusubiri kwanza ili
akaulize ndani endapo wanaruhusiwa kuingia.
Hata hivyo, kabla ya kuondoka kuingia ndani, mlinzi huyo
aliuliza ni aina gani ya bidhaa inayohitaji kununuliwa na waandishi hao; ambao
walisema kwamba wanachohitaji ni tambi za Kichina maarufu kwa jina la Noodles.
Mlinzi huyo, pengine kwa kuhofu kwamba wahusika ni
waandishi wa habari, alitoa ruhusa kwa gari kuingia baada ya kuzungumza na
‘mabosi’ wake ambao walikuwa ni raia watatu wa Kichina; wawili wanawake na
mmoja mwanaume aliyekuwa akipokea malipo.
Mara baada ya waandishi hao kuingia ndani ya duka hilo,
mmoja wa Wachina hao alianza kuzungumza kwa kufoka, akionyesha kuudhiwa na
kitendo cha kuwaona wageni wasiotakiwa kwenye eneo lake la kazi.
Mwanamama huyo alikuwa akifoka kwa kutumia lugha ya
Kichina na wakati mwandishi wa habari hizi alipomhoji mwanaume yule ni kwa nini
mwenzake anafoka mara tu baada ya waandishi kuingia, muuzaji yule hakujibu
zaidi ya kukaa kimya.
Baada ya kumaliza ununuzi, waandishi wetu walikwenda
kufanya malipo lakini kwa kuuliza kwanza kwa nini duka lile halitaki kuhudumia
watu weusi.
“Sielewi Kiingereza sana. Mimi si Meneja hapa na mwenyewe
yuko mbali. Siwezi kuzungumza kwa niaba ya wahusika lakini sijui kama
tunakataza watu weusi wasiingie. Sisi sote ni ndugu kwa nini tufanye hivyo,”
alisema mhudumu huyo wa kiume.
Juhudi za kutaka kuzungumza na yule aliyekuwa akifoka
hazikufanikiwa kwa vile kwanza alikuwa hataki kuonana ana kwa ana, na alikuwa
akiondoka kila alipokuwa akiona dalili ya kutaka kusogelewa na waandishi wetu.
Wahusika wote dukani walionekana kuwa na umri
unaokadiriwa kuwa kati ya miaka 30 hadi 40.
Waandishi wetu waliondoka ndani ya duka hilo lakini
wakati walipokuwa nje na kuchunguza aina ya wateja wanaoruhusiwa, ilibainika
kuwa wageni wazungu na wenye asili ya Kichina walikuwa wakiruhusiwa kuingia
pasipo kuulizwa maswali yoyote na walinzi.
Mmoja wa walinzi waliowahi kulinda duka hilo
alilithibitishia gazeti hili kwamba imekuwa kawaida kwa wamiliki kuwawekea
vikwazo watu weusi kwa sababu ambazo hazijawekwa wazi hadi sasa.
“ Sisi tunapewa maelekezo tu kwamba akija mtu mweusi
aulizwe getini anafuata nini. Akisema mara nyingi tunamwambia hakuna. Mtu
mweusi pekee anayeruhusiwa kuingia ndani ni yule ambaye kafuatana na Mchina.
Bila ya hivyo huingii kabisa,” alisema mlinzi huyo aliyewahi kulinda hapo.
Mlinzi huyo aliliambia gazeti hili kwamba huenda wamiliki
wana wasiwasi kwamba watu weusi wanaweza kuwaibia lakini alipoulizwa na
waandishi wetu kwa nini ni watu weusi pekee wanaoonekana kuwa na uwezekano wa
kuiba kwenye duka hilo na si watu wa asili nyingine, mlinzi huyo wa zamani
hakuwa na majibu.
Alipoulizwa kuhusu tabia hiyo ya wafanyabiashara hao wa
duka la Huarang, Waziri wa Viwanda na Biashara, Dk. Abdallah Kigoda, alisema
alikuwa jimboni kwake Handeni, mkoani Tanga akishughulikia masuala ya kifamilia
na hakuwa katika wakati mzuri kuzungumzia masuala hayo.
Juhudi za gazeti hili kuzungumza na Waziri wa Nchi, Ofisi
ya Waziri Mkuu (Uwekezaji na Uwezeshaji), Christopher Chiza, kuhusu suala hili
hazikufua dafu kwa vile ofisini kwake alielezwa kuwapo ziarani nje ya Dar es
Salaam na simu hakujibu simu wala ujumbe mfupi wa simu aliotumiwa kuomba
kuzungumza.
Watanzania na Wachina wamekuwa wakiishi pamoja hapa
nchini pasipo matatizo, huku Wachina wakifahamika kuwapo Tanzania tangu mwaka
1891 wakati walipoletwa na utawala wa kikoloni wa Wajerumani.
Walikuja nchini kwa wingi zaidi mwishoni mwa miaka ya
1960 wakati wa mradi mkubwa wa ujenzi wa Reli ya Tanzania na Zambia (Tazara)
lakini wamekuja wengi zaidi kwenye miaka ya karibuni, baada ya Tanzania
kufungua milango ya kiuchumi.
Kwa mujibu wa ripoti ya Shirika la Habari la China la
XINHUA ya mwaka 2012, Tanzania inakadiriwa kuwa na raia wa China zaidi ya
10,000.
RAIA MWEMA
No comments:
Post a Comment