Kwa
sababu tu una watoto wadogo nyumbani haimaanishi utashindwa kuiweka nyumba yako
kwenye muonekano nadhifu na wa kuvutia. Nimeongea na mbunifu wa ndani Bi Aisha
Omari ambapo atatujuza jinsi ya kupamba nyumba yako na wakati huohuo ukiwa na
watoto wadogo ndani.
Karibu
Aisha!
“Ukiwa
unaishi na watoto wadogo kuna vitu vinaweza kukuvunja moyo kama vile unarudi na
kukuta meza yako ya kioo imevunjwa,
kochi limemwagiwa tomato sosi na kwa ujumla
nyumba nzima imevurugwa imebadilika”, anasema Aisha. Ndipo hata kabla ya
kupumzika unaanza kusafisha na kupanga upya, kwenye makala hii utafurahia Aisha
atakayotushirikisha.
Kila
nyumba ina utambulisho wa muonekano wake wa ndani tofauti na nyingine. Huenda upo kwenye kipindi
cha mpito nyumbani kwako kutoka mtoto aliyekuwa hajaanza kukaa kwenda kwenye
anayeanza kutambaa na kutembea hadi miaka mitatu; ni kwa namna gani mapambo
yako ya ndani yataendana na kipindi hiki? Ni mabadiliko gani makubwa utayotakiwa
kufanya kipindi hiki?
Wazazi
wenye watoto wadogo huwa wananiuliza kama inawezekana kuwa na nyumba
iliyopambwa vizuri na kuwa na watoto ndani wakati huohuo. Jibu ninalowapa ni
NDIO! Njia zifuatazo zitakuwezesha kupamba nyumba yako na ikawa na muonekano wa
kuvutia hata kama unaishi na watoto wa umri mdogo kabisa.
Sehemu
kubwa ambayo watoto wanapenda kucheza na kuchafua kwa vyakula na vinywaji ni
kwenye viti na makochi. Hata kama utajitahidi kuwazuia namna gani mwishoni hivyo
vita mzazi hutaviweza, utashindwa tu, kwani utatoka na kurudi na kukuta
wameshamwaga kitu kwenye makochi au zuliani. Suluhisho lake ni weka sofa zenye
kitambaa kisichoonyesha uchafu na pia vitambaa hivyo viwe ni vya kuvulika kiasi
kwamba unaweza kuviondoa na kufua.
Mtoto
mdogo anapokuwa anajifunza kutembea na kukimbia huku na huko akiwa ndani ya nyumba
ni hatari kuwa na meza ndogo ya kioo. Kipindi hiki unatakiwa kuwa na mkakati
maalum kwenye mapambo yako ya ndani, kwa mfano usiweke meza ya kioo au yenye
ncha kali, badala yake weka ya mbao ya duara na hata kama utapata zile
zilizoshonewa vitambaa juu itakuwa salama zaidi. Meza ya kioo ina uwezekano
mkubwa wa kuangushwa au kupigwa na kitu na mtoto na hatimaye kuvunjika na
kumuumiza vile vile, ambapo usingependa mapambo yako yamuumize mtoto.
Pia,
watoto wadogo wana nguvu nyingi na wanapenda kupeleleza vitu. Sasa hii
haimaanishi kuwa mapambo yako madogomadogo ya kioo uyafungie. Yahamishe yaweke
juu sehemu ambapo hawafikii. Tumia shelfu za juu kwa kuwekea mapambo ya
kuvunjika na za chini weka yale ambayo hayana shida hata akitaka kuyashika
kupeleleza na atakuwa huru kuchezea. Usiweke mapambo ya kuvunjia kwa mfano vesi
ya maua ya kioo kwenye meza ya kahawa kwa ajili ya usalama wa mtoto.
Sanaa
za ukutani ni moja kati ya njia nzuri zaidi za kuongeza rangi na michoro kwenye
chumba.Ongeza mapambo kwenye zile sehemu ambazo watoto wako wadogo hawafilkii.
Picha za ukutani zilizo juu watoto ambao hawajawa na uelewa hawawezi kuzifikia.
Watoto
wanapenda kuvuta pazia na kujificha nyuma ya pazia. Kwa kufanya hivi wanaweza
kuzing’oa na pia kuzichafua. Suluhisho lake ni kuwa ukiwa na watoto wadogo weka
pazia fupi, zinazopita dirisha kidogo tu, usiweke zile za kuburuza hadi
sakafuni kwa kuwa zitakuwa kishawishi kwao kuzichezea.
Ukiwa
na watoto wadogo ndani zingatia rangi za kuta na zulia. Huenda unapenda rangi
za mwanga lakini mimi Aisha nakushauri kuwa ukiwa na watoto wadogo weka rangi
za kufifia hadi pale watoto watakapokua ndio unaweza kubadili. Kwa mfano ukuta
wa rangi ya kijivu ni bora zaidi kwa watoto kuliko mweupe, hali kadhalika na
zulia vilevile.
Tukiwa
tunajiamini na mapambo ya nyumba zetu inatufanya tupende mahali tunapoishi.
Tunakuwa huru zaidi na kufurahia maisha kwa kiwango kikubwa zaidi, anasema
Aisha. Kwenye kazi yangu ya ubunifu wa ndani nimegundua kuwa watu wengi wanajua
wanachopenda, lakini shida ni jinsi ya kugeuza picha iliyoko kichwa kuwa ya
kweli ndani ya nyumba zao.
Usikose
makala ijayo hapahapa jumamosi ijayo ili upate siri za kufanya makazi yako
yaonekane nadhifu.
Makala
hii imeandaliwa na Vivi, kwa maswali au maoni tembelea www.vivimachange.blogspot.com
No comments:
Post a Comment