CHAMA cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) kimetangaza
kuwa adui yake namba moja ni Kiongozi Mkuu wa Chama cha Alliance for Change and
Transparance (ACT-wazalendo), Zitto Kabwe.
Naibu Katibu Mkuu wa chama hicho Bara, John Mnyika
akihutubia mkutano wa hadhara uliofanyika Uwanja wa Furahisha Mwanza juzi,
alisema Chadema haiko tayari kuikaribisha ACT-Wazalendo ndani ya Umoja wa
Katiba ya Wananchi (Ukawa) kutokana na kile alichosema ‘ni adui kwao’.
“Mtume Muhamad (S.A.W) alikuwa anazungumzia unafiki ambao
una sura mbili na sifa zake, leo (ACT) wanasema wapo upinzani, wanasema msiunge
mkono Ukawa halafu mnawakaribisha?
“Nendeni kila mahali waambieni wananchi adui yetu mkuu ni
Zitto. Sikilizeni niwaambie Taifa hili kama ni ufisadi tumeshazungumzia sana
kuanzia EPA mpaka Richmond. Dk. Slaa (Willbrod) alipoingia bungeni aliyasema
haya kwa sasa si mapya. Adui yetu ni Zitto na hatumtaki Ukawa,” alisema Mnyika.
Alisema Chadema haiko tayari kuikaribisha ACT-Wazalendo
Ukawa kwa sababu adui kwao.
Zitto ajibu
Akihutubia mamia ya wananchi wa Mwanza jana, Zitto
alisema kadri siku zinavyosonga wabaya wake wamekuwa wakijionyesha.
Zitto alisema pamoja na hali hiyo, ACT-Wazalendo haiko tayari
kuzungumzia siasa za wakati uliopita kwa vile kufanya hivyo si afya njema kwa
siasa za upinzani.
Alisema ni vema viongozi wa vyama vya upinzani waachane
na ugomvi binafsi na watangulize masilahi ya taifa mbele.
“Mwanzo walipotufukuza walituambia tukatafute vyama
vingine hilo likafanyika, tulipopata vyama vya kufanyia siasa wakasema vipo kwa
ajili ya kugawa upinzani tukasema tupo tayari kuunganisha nguvu ya pamoja kwa
ajili ya kuiondoa CCM…wenzetu pia hili hawalitaki sasa ni wajibu wenu kutambua
watu gani hawataki kuiondoa CCM,” alisema Zitto.
Alisema wao (ACT) wana nia ya dhati lakini wenzao
wanaweka ugomvi binafsi mbele ya masilahi ya taifa.
“Sisi ACT Wazalendo bado tupo tayari kushirikiana kwa
mujibu wa misingi. Shabaha yetu ni moja tu, kubomoa mfumo wa uchumi wa
kinyonyaji na ufisadi ili kujenga uchumi shirikishi wa wananchi,” alisema na
kuongeza:
“Sikufundishwa kugombana na watu barabarani au kusema
ovyo mitaani, kufanya hivi hakuna tofauti na kumsema mke au mume
mlioachana…mmoja kwa kukosa busara na kwa kuwa aliachana na yule mke anaamua
kwenda vijiweni na kutoa siri za mzazi mwenzie, hili kwetu hapana.
“Tunakuja na jahazi jipya ambalo ndugu zangu wa Mwanza
nimekuja kuwakabidhi, kubwa tunataka kulirudisha taifa katika misingi yake ya
ujamaa na kujitegemea, tunahitaji ujamaa wa demokrasia,” alisema Zitto.
Alisema tafsiri ya ujamaa haina maana kuwa chama hicho
kitataifisha mali za watu, bali kitarekebisha makosa ya ubinafsishaji kwa
kurejesha mali zote za taifa zilizouzwa na wanunuzi hawajatekeleza mikataba
yao.
Mapokezi
Zitto ambaye amefuatana na Mwenyekiti wa chama hicho,
Anna Mghwira, waliwasili Mwanza saa 8.00 mchana na kupata mapokezi makubwa
yaliyoanzia wilayani Misungwi.
Mapokezi hayo yaliongozwa na vijana waendesha pikipiki
(bodaboda) na kikundi cha wanawake ambao muda wote walikuwa katika shamrashara
hadi alipoingia kwenye uwanja wa Furahisha.
MTANZANIA
No comments:
Post a Comment