Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), kimeshika nafasi ya
kumi miongoni mwa vyuo vikuu 50 bora na vyenye umaarufu Afrika.
Kadhalika UDSM kimetajwa kuwa miongoni mwa
chuo vikuu chenye
idadi kubwa ya wanafunzi na walimu na wingi wa programu za masomo.
Makamu Mkuu wa chuo hicho, Profesa Rwekaza Mukandala
alisema chuo hicho kina haki ya kushika nafasi hiyo kutokana na jitihada
zinazofanywa na uongozi.
“Tulifanya jitihada kuhakikisha tuna walimu wazuri wenye
shahada za uzamili na uzamivu, maabara nzuri na miundombinu rafiki ya
kufundishia,” alisema Mukandala.
Alisema UDSM ina mitaala bora inayoendana na wakati na
inazalisha wataalamu wengi kwa mwaka.
“UDSM inachaguliwa na wanafunzi wengi na pia ina
wanafunzi wa kimataifa,”alisema.
Katika matokeo ya utafiti huo uliofanywa na Taasisi ya
Kimataifa ya Vyuo Vikuu na vya Kati (4ICU) ya Uingereza, chuo hicho kilishika
nafasi ya 10 kati ya vyuo 50 vilivyopimwa kulingana na vigezo vya taasisi hiyo.
Hata hivyo, taasisi hiyo ilieleza kuwa hawapimi ubora wa
vyuo kwa kuangalia kiwango cha elimu inayotolewa au huduma bali wanaangalia
umaarufu wa chuo kimataifa.
“Huu mtandao si kwa ajili ya taaluma wala usichukuliwe
kama kipimo cha kuchagua programu au nafasi ya masomo, huu ni kwa ajili ya
kuwasaidia wanafunzi wa kimataifa kufahamu jinsi taasisi ya elimu ilivyo
maarufu katika nchi nyingine,” ilisema taarifa ya 4ICU.
Katika taarifa hiyo, Chuo Kikuu cha Cape Town cha Afrika
Kusini kilishika nafasi ya kwanza huku vingine vilivyoshika tano bora vikitoka
nchini humo.
Nafasi ya pili ilishikwa na Chuo Kikuu cha Pretoria, ya
tatu Chuo Kikuu cha Stellenbosch na nne ilikwenda kwa Chuo Kikuu cha
Witwatersand na tano ikishikwa na Chuo Kikuu cha Afrika Kusini.
Ikieleza namna walivyoweza kupata vyuo bora, tovuti ya
4ICU iliangalia jinsi mitandao mingine inavyozungumza na kutoa taarifa za chuo
husika, nafasi yake katika kurasa za mtandao ya kijamii kutafuta taarifa kwa
google, chuo kinavyotumiwa kama rejea katika taarifa mbalimbali na ni kwa kiasi
gani watu wanaitumia tovuti ya chuo husika.
MWANANCHI
No comments:
Post a Comment