Saturday, April 25, 2015

My article for newspaper: Aina mbalimbali za taa za chumba cha kulala na matumizi yake


Chumba cha kulala ni cha faragha kati ya vyumba vyote ndani ya nyumba. Taa zinaweza kubadilisha muonekano na pia kuwezesha shughuli mbalimbali kufanyika kwenye chumba cha kulala pale jua linapozama.

Iwe unachagua taa za chumba cha kulala cha wakuu wa familia au cha watoto makala hii itakujuza kwa upana kuhusu taa za chumba cha kulala.

Nimeongea na Agnes Mushi ambaye ni mtaalam wa taa za majumbani kwenye duka la kuuza taa na hapa atatufahamisha mengi.

Anasema, chumba cha kulala kiwe kiwavyo ni lazima kinatumika kwa shughuli zaidi ya moja. Vyumba vya kulala vyenye giza ni vizuri kwa usingizi  ila mwanga kidogo sana unazuia shughuli nyingine kuchukua nafasi chumbani hapo. 

Taa za chumba cha kulala zipo za aina kadhaa kutokana na shughuli inayofanyika hapo kwa wakati husika. Kwa maana hiyo Agnes anashauri kuwa kabla ya kununua taa za chumba cha kulala fahamu kwanza ni nini kinafanyika kwenye chumba hicho zaidi ya kulala.

Kwa ajili kama tujuavyo sio kuwa ukiwa bedroom umefumba macho tu, kuna wakati unasoma kitabu au gazeti, kuna wakati unaangali muvi na kama ni mwanafunzi kuna wakati unafanya masomo yako ya shule.

Ukishajua ni nini unafanya ukiwa kwenye chumba chako cha kulala ndipo utakapochagua aina sahihi ya taa. Wapo walio na kompyuta kwenye vyumba vyao vya kulala na pia wapo wanaoshonea mle vilevile.

Hakuna aina moja ya taa itakayowezesha kila shughuli kwenye chumba cha kulala. Mchanganyiko wa aina taa zaidi ya moja ndio unaotakiwa, anasema Agnes. “Ni vyema kuwa na vyanzo vingi vya taa lakini zenye balbu za wati ndogo.”

Taa za kwenye dari kwa maana ya kwamba za juu ni kwa ajili ya kuangaza chumba kizima – zinafaa sana wakati unasafisha ama umepoteza soksi (kicheko). 

Ila Agnes anashauri taa hizi za juu zisikae eneo la dari katikati ya kitanda usawa wa macho yako ukiwa umelala kitandani. Badala yake zikae juu pembeni na hata kama zitakuwa zimefungwa kwenye ukuta ni busara zaidi kwani haifurahishi kufungua macho na kugongana moja kwa moja na mwanga mkali wa taa ya juu ya kitanda. Kwa wale mlioko kwenye ujenzi au maboresho ya nyumbani zingatieni hili.

Kama unasoma kitandani, taa nzuri ni  za kivuli za mwanga wa kurekebishika pembeni mwa kitanda. Hakikisha unatumia balbu zisizokuwa na joto sana. 

Taa hizi zinakusaidia kusoma ukiwa umelala bila kumbughudhi mwezi wako kwa mwanga wa taa. Pia taa hizi za pembeni mwa kitanda za kusomea zinafaa ziwe na kivuli cha kutosha kiasi kwamba balbu yake ya ndani haionekani kwa lengo lile lile la kutokumsumbua aliyelala pembeni yako ambaye hahitaji mwanga kwa wakati huo.

Huenda unawahi kuamka mapema zaidi ya mwenzi wako kuwahi kazini, kama una kabati la nguo chumbani je utavaaje kwenye giza pasipo kumsumbua mwenzako? Suluhisho ni kuweka taa kwenye kabati la nguo, unawasha unaona nguo zako unachagua unayotaka kuvaa.

Taa za namna hii zipo zile ambazo ukifungua kabati zinawaka zenyewe, ukifunga zinazimika bila kuwa na haja ya kuzima na kuwasha mwenyewe, anasema Agnes.

 “Ila kuwa makini usifunge balbu yenye joto kali karibia na nguo laini kwa vile inaweza kuunguza” kabati la nguo linahitaji mwanga wa kutosha ili kuweza kuona vyema rangi za nguo zako, anasema Agnes.

Na kama unavaa gauni la mtoko na vitupio vyake ili kujiamini utaonekanaje suluhisho ni kutumia taa za pembeni mwa kioo.

Kuwa na uhakika una aina sahihi ya taa kwenye chumba chako cha kulala, Agnes anashauri ujiulize maswali haya na uwezo kujijibu ndio yote!

Je, una mwanga wa kutosha kukuwezesha kuvaa nguo unayotaka, kuna taa za pembeni za kusomea na kuna taa ya juu kwa ajili ya mwanga wa chumba kizima?

Upo hapo? Kwahivyo mwisho wa siku kutokana na aina ya maisha unayoishi unajikuta kwenye chumba chako cha kulala kuna taa nyingi tofauti kwa matumizi mbalimbali. Kumbuka unaishi mara moja tu, raha jipe mwenyewe.


Makala hii imeandaliwa na Vivi, kwa maoni au maswali tembelea www.vivimachange.blogspot.com

No comments:

Post a Comment