Muuguzi mmoja wa zahanati ya Muungano, Chamwino, mkoani Dodoma, amekumbwa na kashfa nzito baada ya kudaiwa kumchapa viboko mama mjamzito,
wakati akiwa katika hali ya uchungu wa kujifungua na kusababisha mtoto
aliyetaka kujifungua kufariki akiwa tumboni.
Aidha, mama huyo ambaye kwa sasa amelazwa katika chumba
cha uangalizi maalumu (ICU)
katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Dodoma, hali
yake inaelezwa kuwa mbaya.
Mwanamke huyo, Mariamu Maroda, anadaiwa kulazwa kwenye
chumba hicho kwa zaidi ya wiki moja, ambapo pamoja na kufanyiwa upasuaji,
hakufanikiwa kupata mtoto wake akiwa hai.
Akisimulia mkasa huo, mama mdogo wa Maroda, Joyce
Charles, alisema Aprili 3, mwaka huu Saa 12:00 jioni, walimpeleka zahanati ya
Muungano akiwa na dalili za kujifungua na kupokelewa na muuguzi aliyemfahamu
kwa jina la Lucy.
“Nilishuhudia Lucy akimchapa Maroda viboko kwenye mapaja na
mgongoni, akisema ana uwezo wa kujifungua lakini anadeka tu, nilishindwa
kuingilia nikihofia asimdhuru zaidi mwanangu, ila nilihuzunika sana,” alisema.
Alisema muuguzi huyo alitumia fimbo tatu kumchapa mgonjwa
wake, ambazo alikuwa akizitumia kila moja inapovunjika. Alisema fimbo hizo
zilipomalizika, alianza kumfinya kwenye mapaja kwa kutumia rula.
“Kesho yake saa 12:00 alfajiri, huku hali ya mgonjwa
ikiwa mbaya, walitupatia gari likatupeleka hospitali ya Mvumi Misheni, ambako
walisema hali aliyokuwa nayo mgonjwa wasingeiweza na kutuelekeza tumpeleke
hospitali ya rufaa, lakini walimpa mgonjwa chupa mbili za damu,” alisema.
Alisema Maroda alifikishiwa chumba cha upasuaji na kisha
alilazwa wodi namba 17, lakini miguu na tumbo vilianza kuvimba na
alipochunguzwa ikabainika ana usaha tumboni, hivyo aliamriwa arudishwe kwenye
chumba cha upasuaji.
“Yaani ukimuona, mwilini ana alama za fimbo na kufinywa.
Sasa walipomfanyia upasuaji kwa awamu ya pili, alipelekwa ICU mpaka hivi
tunavyozungumza ni zaidi ya wiki moja,” alieleza Charles.
Viongozi wa Hospitali ya Rufaa, wenye mamlaka ya
kuzungumzia suala hilo walionekana ‘kurushiana mpira’ walipotakiwa kuelezea
suala hilo. Hata hivyo, Muuguzi Mkuu wa Mkoa wa Dodoma, Anatoria Mkindo,
alikiri kuwepo kwa mgonjwa huyo.
Awali Kaimu Mganga Mfawidhi wa hospitali hiyo, Dk. Zainab
Chaula, alisema hakuwa na taarifa za kina kuhusu Maroda.
Mkindo alisema walikuwa wameagiza Ofisi ya Mganga wa
Wilaya wa Chamwino, kuwapelekea taarifa kuhusu suala hilo.
Alisema pia wametaka Ofisi ya Mganga Mkuu wa mkoa,
ifahamishwe hatua zilizochukuliwa dhidi ya mtumishi aliyedaiwa kumchapa viboko
mjamzito huyo.
“Mimi sio msemaji, anayetakiwa kuwapa taarifa kamili ni
RMO (Chaula) kwanini awalete kwangu, nilichowaeleza ni ambacho nafahamu lakini
siyo msemaji, nashauri muende ofisini kwa matroni wa hospitali mtapata taarifa
kamili,” alisema.
Afisa Muuguzi wa ICU, Christina Mlumba, alisema, Maroda
alipelekwa ICU baada ya kufanyiwa upasuaji na kwamba hali yake inaendelea
vizuri.
Mdogo wa Maroda, Silika Mkwawi alivieleza vyombo vya
habari kuwa ingawa hakuingia kwenye chumba cha kujifungulia katika zahanati ya
muungano, dada yake alipotolewa nje, muuguzi alimueleza kuwa alimchapa fimbo
mbili tu, kwa sababu ya kudeka kwake.
CHANZO: NIPASHE
No comments:
Post a Comment