Sheikh Mkuu wa Tanzania, Mufti Issa Bin Shaaban Simba,
amevitaka vyombo vya dola kufuatilia kwa makini baadhi ya misikiti inayodaiwa
kutumiwa na baadhi ya waumini wake kufanya mazoezi nyakati za usiku.
Akizungumza na
JAMHURI katika mahojiano maalum yaliyofanyika hivi karibuni, Mufti alionesha
kushangazwa baada ya kusikia kuwa kuna baadhi ya misikiti nchini imekuwa
ikitumika kufanyia mazoezi usiku baada ya ibada.
Akizungumza kwa
umakini, Mufti Simba anasema kuwa hilo ni jambo la ajabu maana hakuna mahali popote
katika dini ya Kiislamu inakoelekeza hivyo.
Anasema hafahamu
kama nyumba hizo za ibada zinatumika kwa ajili ya kufanyia mazoezi, lakini siyo
sahihi kutumika kwa ajili ya kufanyia mazoezi nyakati za usiku.
Mufti Issa Bin
Shaaban Simba anahoji sababu za waumini hao kufanya mazoezi katika misikiti
nyakati za usiku, huku wakijua wazi kuwa hakuna mahali popote vitabu vitakatifu
(Quran) vilipoelekeza kufanya hivyo.
“Haya mambo
hayatokani na taratibu za dini ya Kiislamu, hili jambo siyo sahihi kabisa,
hatuna utaratibu huo katika miongozo ya dini yetu, hapa ipo haja ya vyombo vya
ulinzi na usalama kutazama na kufuatilia kwa makini hawa wanaofanya hivyo ni
kina nani na wana dhamira gani!” anasema Mufti Simba.
Anabainisha kuwa
Waislamu wana shule wanazomiliki, na katika shule hizo hakuna hata moja
inayofundisha kufanyika kwa mazoezi katika nyumba za ibada, bali kama
wanahitaji kufanya mazoezi ya viungo huyafanya katika viwanja vya wazi na
nyakati za mchana na si usiku.
“Mimi binafsi nashindwa kabisa kuliongelea hili kwa
undani maana halipo kwenye imani zetu, pia misikiti inayofanya hivyo siifahamu
ila ni vyema vyombo vya dola vikawa makini na hili ili kujiridhisha na kuchukua
hatua ikibidi,” anasema Mufti.
Kwa upande wake,
Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Mathias Chikawe, anaeleza kuwa ni vyema
nyumba za ibada zikatumika kwa shughuli za ibada tu na si vinginevyo.
Chikawe
aliyezungumza na gazeti hili, anasema kuwa msikiti ni nyumba ya kufanyia ibada,
ni mahala patakatifu hivyo haiwezekani kuigeuza kuwa nyumba za kufanyia mazoezi
(gym) kama ambavyo inafanywa na baadhi ya watu.
Pia alihoji
sababu za kufanyika kwa mazoezi hayo katika nyumba hizo za ibada. “Wanajifunza
karate na kupigana ili iweje? Wanataka kupambana na nani hasa? Tena wanafanya
kwa kificho, nyakati za usiku ndani ya nyumba za ibada ili itokee nini?”Anasema
na kuongeza: “Kama wana nia njema, basi hawana sababu za kufanya mazoezi hayo
usiku tena kwenye nyumba za ibada”.
Hata hivyo,
alilitaka gazeti hili kuwasiliana na Mkuu wa Jeshi la Polisi nchini (IGP),
Ernest Mangu, ili kupata ufafanuzi wa kina kuhusiana na suala hilo.
IGP Mangu
akizungumzia sakata hilo, anaeleza kuwa jeshi hilo linahusika na makosa ya
jinai, hivyo anaomba kupatiwa orodha ya nyumba hizo za ibada zinazojihusisha na
kufanya mazoezi hayo ili Jeshi la Polisi liweze kufuatilia.
“Tuleteeni majina
ili tufuatilie tuweze kujua ni mazoezi gani yanayofanywa humo nyakati za usiku,
kama ni kosa la jinai tutakuja tuseme, kwa sasa siwezi kukwambia lolote bali
nipe majina… inaonekana kuna kitu mnajua zaidi,” anasema Mangu.
Wiki iliyopita,
watu 10 walikamatwa katika msikiti wa Sunni uliopo Kidatu, Wilaya ya Kilombero,
wakituhumiwa kuhusika na vitendo vya ugaidi.
Watu hao
walikamatwa baada ya wasamaria wema kuliarifu Jeshi la Polisi kuhusu uwepo wa
watu wanaojihusisha na vitendo vya uhalifu katika msikiti huo.
Mmoja wa viongozi
wa Msikiti wa Masjid Salah Al-Fajih, Mohamed Manze, anasema kuwa wao kama
viongozi na waumini msikitini humo hawakuwa na taarifa zozote za ujio wa
watuhumiwa hao, na kwamba wapo vijana wanne tu ambao wamekuwa wakilala na
kujisomea msikitini humo.
Kiongozi huyo
anasema kuwa hawakupendezwa na suala hilo na kwamba limewachafua na kuwaharibia
sifa waumini wa msikiti huo.
Katika tukio
hilo, Hamadi Makwendo aliuawa kwa kupigwa risasi na askari baada ya kumjeruhi
askari kwa kumkata kwa jambia.
JAMHURI MEDIA
No comments:
Post a Comment