RAIS Jakaya Kikwete ametoa msamaha kwa wafungwa 4,129
ambako 400 wataachiwa huru na wengine 3,729 watapunguziwa vifungo vyao.
Alitoa msamaha huo katika kuadhimisha miaka 51 ya
Muungano wa
Tanganyika na Zanzibar, kwa kutumia madaraka yake aliyopewa chini
ya Ibara ya 45(1)(d) ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano.
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Wizara ya Mambo ya
Ndani ya Nchi na kusainiwa na Katibu Mkuu wa wizara hiyo, Mbarak Abdulwakil,
wafungwa waliopunguziwa vifungo watabaki gerezani wakitumikia sehemu ya kifungo
kilichobaki.
“Ni mategemeo ya Serikali kwamba wafungwa watakaoachiwa
huru watarejea katika jamii kushirikiana na wananchi wenzao katika ujenzi wa
taifa na watajiepusha kutenda makosa ili wasirejee tena gerezani,”ilisema
taarifa hiyo.
Katika msamaha huo wafungwa wote watapunguziwa moja ya
sita ya vifungo vyao zaidi ya punguzo la kawaida linalotolewa chini ya kifungu
namba 49(1) cha Sheria ya Magereza sura ya 58, isipokuwa wafungwa wenye makosa
yasiyo na msamaha.
Wafungwa waliosamehewa ni wenye magonjwa kama Ukimwi,
kifua kikuu na saratani, wafungwa wazee wenye umri wa miaka 70 au zaidi na
wafungwa wa kike walioingia na mimba gerezani na wale walioingia na watoto
wanaonyonya na wasionyonya.
Wengine ni wafungwa wenye ulemavu wa mwili na akili. Wote
waliosamehewa wanatakiwa kuthibitishwa na jopo la waganga chini ya uenyekiti wa
mganga mkuu wa mkoa ama mganga mkuu wa wilaya.
Kwa mujibu wa taarifa hiyo, wafungwa ambao hawakupata
msamaha ni waliohukumiwa adhabu ya kunyongwa, kifungo cha maisha, wanaotumikia
kifungo kwa makosa ya kujihusisha na uombaji, upokeaji au utoaji wa rushwa.
Wengine ni wanaotumikia kifungo kwa unyang’anyi, makosa
ya kupatikana na silaha, makosa ya shambulio la aibu, kunajisi, kubaka na
kulawiti au kujaribu kutenda makosa hayo.
Pia wale waliowapa mimba wanafunzi wa shule za msingi na
shule za sekondari na ambao walitenda makosa hayo wakiwa na umri wa miaka 18.
Wezi wa magari na pikipiki, kutumia vibaya madaraka,
waliowahi kupunguziwa kifungo na msamaha wa Rais, waliozuia watoto kupata
masomo, utekaji wa watoto, kufanya biashara ya binadamu, kukutwa na viungo vya
binadamu pamoja na vitendo vya ukatili na mashambulio dhidi ya albino.
MTANZANIA
No comments:
Post a Comment