Saturday, April 18, 2015

Watu Zaidi ya 100 Wanahofiwa Kufa Baada ya Kuangukiwa na Kifusi Katika Machimbo ya Dhahabu ya Wachimbaji Wadogowadogo Katika Kijiji cha Kalole Wilayani Kahama

Watu zaidi ya mia moja wanahofiwa kufa baada ya kuangukiwa na kifusi katika machimbo ya dhahabu ya wachimbaji wadogo wadogo ya kalole yaliyoko katika kata ya msalala wilayani kahama mkoani shinyanga na inasemekana wachimbaji hao walivamia mgodi baada ya muda wa kazi hali iliyosababisha mashimo manane ya mgodi huo kutobozana na hatimaye nguzo kuvunjika na kisha kifusi kuwaangukia.

ITV ilifika katika eneo hilo
na kukuta zoezi la kutambua maiti linaendelea na wakaguzi wakiendelea na zoezi la kukagua mashimo yaliyokuwa wazi huku baadhi ya wachimbaji walionusurika katika tukio hilo wakiulalamikia ulinzi wa machimbo hayo kuwa ndio chanzo cha tukio hilo kwakuwa tukio lilitokea mapema saa kumi na mbili baada ya saa za kazi lakini inashangaza taarifa kupatikana saa sita za usiku na wamedai kuwa idadi ya watu waliofukiwa na kifusi ni zaidi ya mia na hamsini lakini serikali imeridhika na idadi ya watu kumi na tisa ambao wameshaopolewa hadi wakati huu.

Akithibitisha kutokea kwa tukio hilo kamanda wa jeshi la polisi mkoa wa shinyanga Justus Kamugisha amesema watu hao walivamia mgodi baada ya muda wa kazi kuisha na kulingana na wingi wao mgodi ulielemewa na kusababisha nguzo kuvunjika hali iliyosababisha kifusi kuwaangukia lakini kwa jitihada za jeshi la polisi tayari wameshaopolewa watu kumi na tisa na kumi na mbili kati yao wameshatambuliwa na tayari wameshachukuliwa na ndugu zao tayari kwa maziko.


Kwa upande wake mkuu wa wilaya ya kahama Bw. Benson Mwampesya amesema kwakuwa imeonekana idadi ya vijana walioangukiwa na kifusi ni wengi zaidi ya hao walioopolewa serikali imeamua kuomba wataalam na mitambo ya kuchimba eneo hilo kutoka katika mgodi wa bulyanhulu unaomilikiwa na kampuni ya acacia ili kuharakisha zoezi la kuhakiki kuwa hakuna maiti zingine zilizonaswa katika mashimo ya mgodi huo.

No comments:

Post a Comment