Mwanafunzi wa kidato cha pili katika Shule ya Sekondari
Matui, amefariki dunia darasani baada ya kudaiwa kuchapwa viboko
na walimu watatu wa shule hiyo, kwa kile kilichodaiwa kufeli mtihani wa
Kiswahili.
Polisi wilayani na mkoani Manyara,
wanamshikilia mwalimu
mmoja baada ya wenzake kukimbia baada ya tukio.
Akizungumza jana, Mkuu wa Wilaya ya Kiteto, Kanali Samwel
Nzoka alimtaja mwanafunzi huyo aliyepoteza maisha kuwa ni Noel Bichima (15).
Kanali Nzoka alisema tukio hilo lilitokea juzi asubuhi
wakiwa darasani, wakati mwalimu huyo anayeshikiliwa na polisi alipokuwa akiwafundisha.
Inadaiwa mwanafunzi huyo alichapwa viboko vinane. Haikuelezwa kama alichapwa
kiganjani ama sehemu nyingine.
Nzoka alidai kuwa mwalimu huyo alimchapa marehemu baada
ya kupata alama 40 katika mtihani wa somo la Kiswahili kwani walipeana mkakati
wa kutofeli na kwamba mwanafunzi atakayepata chini ya alama 40 atachapwa fimbo
12.
“Mwanafunzi huyo alifariki dunia papo hapo darasani baada
ya kuanguka chini alipochapwa viboko na walimu hao na mwili wake umehifadhiwa
kwenye Hospitali ya Wilaya ya Kiteto ukisubiri uchunguzi,” alisema Kanali
Nzoka.
“Natoa wito kwa walimu wa shule za msingi na sekondari,
kuangalia namna ya kutoa adhabu kwa wanafunzi wanapokosea, baadhi ya watoto
afya zao siyo nzuri,” alisema Kanali Nzoka.
Diwani wa Kata ya Matui, Athumani Kidawa alisema baadhi
ya wazazi wa eneo hilo waliopatwa na hasira baada ya kutokea tukio hilo,
waliandamana hadi Kituo cha Polisi Matui kulalamikia kitendo hicho.
MWANANCHI
No comments:
Post a Comment